NA AMEIR KHALID, MTWARA

WACHEZAJI wanane wa timu ya soka ya UMISSETA kanda ya Unguja huenda wakatapa fursa ya kuchukuliwa na vituo mbali mbali vya soka la vijana Tanzania bara.

Taarifa za ndani ya timu hiyo zilizopatikana na mwandishi wa habari hizi, zinaeleza kuwa tayari mazungumzo ya awali baina ya vijana hao na kocha wa timu hiyo yamefanyika.

Hivyo kinachosubiriwa hivi sasa ni viongozi wa vituo hivyo kufanya mazungumzo na wazee, walimu wa skuli walizotoka na viongozi wa timu wanazochezea ili kukamilisha taratibu za kuwachukua rasmi.

Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa timu hiyo, viongozi wa vituo (academy) hivyo wamefikia uamuzi wa kuwataka vijana hao baada ya kuridhishwa na viwango walivyoonesha katika mashindano ya UMISSETA yanayoendelea mkoani Mtwara licha ya kanda ya Unguja kushindwa kuingia hatua ya robo fainali.

Kiongozi huyo aliwataja vijana hao hao kuwa ni mshambuliaji Abdulhafidh Abuubakar (Kibobea) na beki wa kulia Mahadhi Juma Mahadhi waliochaguliwa na kituo cha Magnet Youth Sports Academy cha jijini Dar es Salaam.

Wengine ni kiungo mkabaji Ibrahim Juma Ali (Janja), mshambuliaji Mohammed Abdalla (Kijeshi), kiungo mshambuliaji Ikram Ali (IKI) na  beki wa kati Abdulhamid Ali Mwalimu (Suso) wote wanaweza kujiunga na kituo cha Fountain Gate Academy cha Dodoma.

Mtoa habari huyo, aliwataja wachezaji wengine kuwa ni mshambuliaji Suleiman Idrisa Suleiman (Sele Messi) na beki wa kushoto Ali Saleh Machupa ambao wameonesha kuwavutia viongozi wa Cambiasso Sports Center ya Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili kocha wa timu hiyo Mohammed Mrishona Mohammed (Xavi), alisema endapo wacheazji hao watajiunga na vituo hivyo, atakuwa ametimiza moja ya melengo aliyojiwekea.