Wasema licha ya uzuri wake bado haijafanya kazi kwa misingi ya kijinsia, jumuishi
Wasema mara zote tume yaongozwa na Mwenyekiti mwanamme
NA HUSNA MOHAMMED
KILA raia katika nchi hii anastahili kupata haki zake za msingi za kila siku awe mtu mwenye ulemavu au asiye na mlemavu, Mwanamke na mwanamme, watoto, wazee na vijana.
Hivyo basi panapozungumzwa haki ni kwamba makundi yote yana haki katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa mfano katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar zimezungumzia waziwazi haki za msingi kwa raia wote bila ya ubaguzi.
Hivi karibuni Wanaharakati na wadau wa masuala ya wanawake na watoto Zanzibar walipitia Sera ya Jinsia na Ujumuishi ya Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kutoa mapungufu yaliyomo sambamba na kupendekeza baadhi ya mambo kufanyiwa kazi na ZEC kwa lengo la kuleta uwiano wa kijinsia.
Katika makala haya Wadau / wanaharakati na watetezi hao wa haki za Wanawake, Vijana na Watoto waliiomba Tume ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ishirikishe wajumbe wengine kutoka sekta mbali mbali zikiwamo asasi za kiraia ili kuangalia, kujadili, kushauri na kupendekeza utendaji mzuri wa usimamizi wa mchakato mzima wa uchaguzi na mwenendo wa vyama vya siasa.
Utafiti mdogo wa kupitia Sera ya Jinsia na Ujumiushi (Gender and Social Inclusion Policy) ya (ZEC) ya mwaka 2015 umebaini kuweko kwa mapungufu yaliyosabisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoshiriki ipasavyo katika mchakato wa chaguzi zilizopita.
TAMWA ZANZIBAR
Akitoa mapendekezo yake Dk Mzuri Issa, ambae ni Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA), alisema kuwa utekelezaji wa sera hiyo haikuzingatia kabisa wanawake kwa kuwa kila kwenye kitengo wanawake ni kidogo ukilinganisha na wanaume.
“Kwa mfano Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi hajawahi kuwa mwanamke, ni makamu amewahi kutokea kwa nafasi hiyo na kati ya makamishna saba nafasi huwa ni moja tu kwa mwanamke katika vipindi vyote vya tume hiyo”, alisema Dk, Mzuri.
Sambamba na hilo, lakini alisema kuwa kiujumla wake tume hiyo imekuwa na watendaji wengi wanaume kuliko wanawake jambo ambalo mambo mengi yanayowahusu wanawake hutatuliwa na wanaume hasa katika mchakato mzima wa uchaguzi.
“Wanawake, vijana, watu wenye ulemavu wanakosa nafasi katika uandikishaji, na mambo yote ya uchaguzi jambo ambalo linnahitaji kuangaliwa kwa umakini hasa katika uteuzi na uajiri”, aliongeza Dk. Mzuri.
“Lazima kuwe na mwongozo maalum katika kila hatua ya uchaguzi kuanzia uandikishaji, utoaji wa elimu ya uraia, uteuzi wa wagombea, usimamizi wa uchaguzi, upigaji kura, utoaji wa matokeo na hali ya usalama na kwamba suala la usawa wa kijinsia na ujumuishi liongoze mchakato wote wa uchaguzi kabla, wakati na baada”, aliongeza Dk. Mzuri.
ASASI YA VIJANA ZANZIBAR WANAZUNGUMZAJE (ZYF)
Dadi Kombo, alisema kuwa sera hiyo si rafiki sana kwa kuwa kwenye Makamishna hakuna kijana ambae yuko katika nafasi hizo muhimu za juu.
“Kundi la vijana ndilo kubwa na la wanawake hapa Tanzania mbali na zile nafasi za muda za tume hasa wakati wa uchaguzi basi makundi hayo mawili hakuna yanavyofaidika kwa kuwa nafasi nyingi zimehodhiwa na wanaume na watu wa rika kubwa”, alisema.
Alisema kama wao wadau walibaini mapungufu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na mwongozo na mpango mkakati wa kuitekeleza sera ya jinsia na ujumuishi ambayo imeundwa maalum kwa ajili ya kuangalia ujumuishi na haki za kijinsia.
Aidha alisema, vijana na watu wenye ulemavu zinazingatiwa katika mchakato mzima wa uchaguzi ili demokrasia siyo tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka.
Dadi alisema ili kuhakikisha usawa wa kijisia na ujumuishi unafikiwa kwa kila hatua ya uchaguzi ZEC inapaswa kukutana na wadau wa masuala ya jinsia, vijana na watu wenye ulemavu mara kwa mara ili kuona hali ikoje na kuweka mpango wa utekelezaji ili pia kusaidia katika ukusanyaji wa takwimu kama sera ilivyosema kuwa ZEC itakuwa na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa takwimu (Systematically Data Collection).
JUMUIYA YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU ZANZIBAR (JUWAUZA)
Mwenyekiti wa JUWAUZA Bi Salma Saadat alisema pia katika utafiti wamebaini uwepo wa kamati ya maadili ya ZEC ni wa muda mfupi, huundwa wakati wa uchaguzi na uhai wake humalizika mara tu baada ya uchaguzi kwisha.
Aidha alisema kamati hiyo haijawekewa mwongozo wa kushughulikia malalamiko wala haina mwongozo wa kutatua vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakati wa uchaguzi.
“Kuna wanawake walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wakati wa uchaguzi lakini hawajui waende wapi kupeleka kesi zao, kwa sababu kamati haina mwongozo wa kutatua kesi za mtu mmoja mmoja, kamati inapokea kesi za vyama vya siasa tu kwa mfano kesi ya ACT Wazalendo kuhusu kiongozi wao kupinga kuwapo kwa kura za mapema ambapo alituhumiwa kuvuruga amani,” alisema Salma.
Hivyo alipendekeza sera hiyo iweke mwongozo na mpango kazi ili ikidhi haja kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika mchakato mzima wa uchaguzi kama wapiga kura, wagombea, wafuatiliaji ilani na sera za vyama na hata kuhakikisha kuwa usalama wao unalindwa vyema.
“Waajiriwa watu wenye ulemavu ni kidogo sana, halafu licha ya kutolewa vitambulisho katika mchakato mzima wa uchaguzi lakini mambo mengi yanayowahusu walemavu hayakuzingatiwa ikiwa ni katika kampeni, kupiga kura mpaka matokeo”, alisema Saadat.
Mapema akiwasilisha mapendekezo ya sera ya jinsia unaohusu tume ya uchaguzi, Haura Shamte kutokea JUWAUZA, alisema kuwa sera ya Tume ya uchaguzi ni nzuri sana nay a kupigiwa mfano si kwa Afrika hata duniani kwa ujumla.
Alisema nchi kadhaa zimekopi namna ya uzuri wa sera ya Tume ya uchaguzi Zanzibar, lakini utekelezaji wake bado ni mdogo ukilinganisha na uzuri wake.
“Sera yetu ya uchaguzi Zanzibar ni nzuri, lakini haitekelezwi hivyo tutapeleka mapendekezo yetu ikiwa ni pamoja na kutaka makamishna wa tume kuongezeka idadi ya wanawake”, alisema.
Aidha alisema kuwa wanakusudia kuishawishi tume kungalia nafasi mbalimbali kama za rasilimali watu juu ya kuwashirikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hasa ikizingatiwa kuwa ni taasisi muhimu inayowagusa watu wengi.
MTANDAO WA JINSIA ZANZIBAR (ZGC)
Asha Aboud Mzee ambae ni Mwenyekiti wa Mtandao wa jinsia Zanzibar (ZGC) alisema wakati umefika sasa tume kuitathmini sera hiyo namna ya ufanyaji kazi wake.
Alisema yapo mambo mengi yanayohitaji kuhimizwa utekelezwaji wake jambo ambalo litaonesha namna ya ushiriki wa makundi yote katika tume ya uchaguzi.
“Wanawake, vijana, watu wenye ulemavu wanakosa nafasi katika mambo yengi na yanapokuwa hayo ni ya muda mfupi tu hivyo tunaomba sera hii itekelezwe kwa udhati kabisa na kuwekwa takwimu sahihi za ushiriki wa makundi hayo”, alisema.
Aidha Wadau wamependekeza Sera ya Jinsia na Ujumishi ya ZEC ipitiwe tena pamoja na kuipangia mpango kazi ili iweze kutekelezeka, jambo ambalo litaweka fursa sawa kwa makundi yote.
KUFANYIWA MAREKEBISHO YA KATIBA
Vile vile katika mapendekezo wadau wameomba katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ifanyiwe marekebisho ili wanawake waweze kuteuliwa kwenye nafasi ya Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa sababu katiba iliyopo sasa haimlazimishi Rais wa Zanzibar kuzingatia usawa wa jinsia wakati wa kuteua Makamishna wa Tume ambapo kwa sasa ZEC ina kamishna mmoja tu mwanamke na sita ni wanaume ikiwa ni sawa na asilimia 14 tu.
“Tunafahamu kuwa mamlaka ya uteuzi wa makamishna siyo wa ZEC kwa kuwa imeainishwa katika Katiba ya nchi kwamba mwenyekiti na wajumbe wengine wawili watateuliwa na rais, ambapo kati ya hao lazima mmoja awe jaji na wajumbe wengine wanne watatoka katika vyama vya siasa.
“Ili kuhakikisha kwamba ZEC inasimamia vyema Sera yake ya Jinsia na Ujumuishi ilisema kwamba mara kwa mara itakua inapendekeza kufanya marekebisho ya katiba ili masuala ya jinsia na ujumuishi yaingie katika katiba na kuifanya sera hii itekelezeke, hivyo tunashauri hatua hiyo ifanywe mapema iwezekanavyo kabla ya uchaguzi mkuu mwingine kwa sababu kumalizika kwa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi mwingine,” alisisitiza Bi Asha Aboud.
BARAZA LA WAWAKILISHI / BARAZA LA MAWAZIRI ZANZIBAR

Hadi sasa Baraza la wawakilishi Zanzibar lina jumla ya wajumbe 79 kati yao wanaume 50 na wanawake 29 ambao kati ya hao wanawake wanane wanatoka majimboni wanne kutoka kisiwa cha Unguja huku wanne wengine wakitokea Pemba ambapo hao 29 ni sawa na asilimia 36.7.
Kwa upand wa baraza la mawaziri hadi sasa mawaziri wote 16 kati ya hao wanaume ni 11 huku wanawake wakiwa ni watano sawa na asilimia 32.
SHERIA NA MIKATABA MBALIMBALI YA KIMATAIFA
Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bado haijatekeleza vyema matakwa ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1982 juu ya haki na fursa sawa kwa baadhi ya mmabo hasa nafasi za wanawake katika serikali na vyombo vya maamuzi.
Hayo yalikuja baada ya wanawake wengi kunyimwa fursa ya kupata nafasi ya kugombea majimboni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hata hivyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akiwachagua wanawake kama alivyoahidi katika teuzi zake mbalimbali za nyadhifa za juu serikalini.
Kwa mfano Ibara ya 8 kifungu cha 111 (b) kinasema ni lazima kukuza katika ngazi zote za mfumo wa elimu, ikijumuisha watoto wote wakiwa na umri mdogo, ikiheshimu haki za watu wenye ulemavu.
Pia ibara hiyohiyo kifungu cha 4 kinasema ili kuhakikisha haki hii inapatikana nchi zilizoridhia mkataba zitachukua hatua zinazofaa kuajiri watu maalumu, wakiwemo watu wenye ulemavu wenye utaalamu na mkundi mengine ya pembezoni.
Aidha kifungu cha 5 kinaeleza nchi zilizoridhia mkataba zitahakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kupata haki yao ya kiraia ikiwemo hilo la kuchagua na kuchaguliwa bila ya ubaguzi kwa misingi sawa na wengine, ili kufikia hatua hii nchi zilizoridhia mkataba zitahakikisha kwamba mahitaji ya watu wenye ulemavu yanashughulikiwa.
Nayo sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar ya nambari 9 ya mwaka 2006 kifungu nambari 9 kinachozungumzia haki ya raia kinasema kuwa watu wenye ulemavu watakuwa na haki sawa ya kupata haki za msingi na za kiraia mafunzo kwa mpango uliowekwa na kufaidika na utafiti kama ilivyo kwa raia wengine.
Kimsingi mengi ya hayo hayajafanikiwa hasa kutokana na kukosekana kwa sera ya watu wenye ulemavu Zanzibar kwa muda mrefu sasa kwani bila ya sera sheria haitoweza kufanya kazi vizuri.
Hivyo, ili kuleta mabadiliko, Serikali inahitaji kuchukua juhudi za makusudi kuyafikia makundi maalumu kwa haki zao zote za msingi na kikatiba ili kufaidika na mambo mbalimbali hapa nchini.
Wadau waliokutana kujadili sera hiyo ya jinsia ya ZEC ni pamoja na Mtandao wa Jinsia Zanzibar (ZGC), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya inayojihusisha na Kupambana na Changamoto zinazowakabili Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Jumuiya ya Vijana Zanzibar (ZYF) na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ).