ADDIS ABABA, ETHIOPIA
VYOMBO vya habari vimetangaza kuwa, wakimbizi wa Kiethiopia zaidi ya elfu tatu wamewasili Sudan katika kipindi cha siku moja kufuatia mapigano yanayoendelea Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Shirika rasmi la habari la Sudan limeripoti kuwa, viongozi wa mkoa wa al Qadarif mashariki mwa nchi hiyo waliwapokea na kuwapa makaazi ya muda wakimbizi wa Kiethiopia wapatao elfu tatu ambao walikimbia mapigano kaskazini mwa Ethiopia.
Idadi hiyo ya wakimbizi wa Kiethiopia ilitajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kuwasili katika ardhi ya Sudan tangu mwezi Novemba mwaka jana baada ya kuanza mapigano kati ya jeshi la Ethiopia na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Eneo la Tigray (TPLF).
Hadi sasa wakimbizi wa Ethiopia elfu 78 walivuka mpaka wa nchi yao na kuingia Sudan.
Mapigano kati ya serikali jeshi la Ethiopia na waasi wa harakati ya TPLF yalianza mwezi Novemba mwaka jana.
Hadi sasa mapigano hayo yaliwalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.