NA AMEIR KHALID
UONGOZI na wanafunzi wa skuli ya Sky View wamesema wataendelea kudumisha usafi wa mazingira katika eneo la skuli na mitaa ya jirani ili kujikinga na maradhi ya mripuko ikiwemo kipindupindu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa skuli hiyo, Ameir Hassan Ameir, alisema lengo la kufanya usafi hivyo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda afya za watu wake.
Alisema serikali imetoa chanjo ya maradhi ya kipindupindi kwa wananchi, lakini lengo hilo haliwezi kufanikiwa vyema endapo mazingira ya wananchi wanayoishi yatakuwa machafu.
Pia alisema lengo jengine ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuweka mazingira ya mji kwenye hali ya usafi, hasa ikizingatiwa kuwa suala la usafi linalomuwajibikia kila mtu.
Diwani wa kuteuliwa Magharibi ‘B’, Thuwaiba Jeni Pandu, aliupongeza uongozi na wanafunzi wa skuli hiyo kwa kuendesha zoezi hilo.
“Hivi karibuni serikali ilitoa chanjo ya maradhi ya kipindupindu ambayo chanzo chake ni uchafu, hivyo zoezi hili limekuja wakati muafaka,” alieleza Diwani huyo.