TUNIS, TUNISIA
WAHAMIAJI wasiopungua 17 raia wa Bangladesh wamezama kwenye bahari ya Tunisia baada ya boti waliopanda kupasuka wakati wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterranean kwenda Italia wakitokea Libya.
Kituo cha Shirika la Mwezi Mwekundu cha Tunisia kimeeleza kuwa Katika ajali hiyo watu zaidi ya 380 waliokolewa na vikosi vya baharini.
Taasisi hiyo ya misaada ya kibinadamu imeeleza kuwa boti hiyo ilikuwa imeanza safari kutoka Zuwara, pwani ya kaskazini magharibi mwa Libya, ikiwa imewabeba wahamiaji kutoka Syria, Misri, Sudan, Eritrea, Mali na Bangladesh.
Ofisa wa mwezi mwekundu Mongi Slim alisema watu 17 walifariki dunia na wahamiaji zaidi ya 380 waliokolewa katika mashua iliyokuwa ikitoka Zuwara ya Libya kuelekea Ulaya.
Katika miezi ya hivi karibuni, watu kadhaa wamezama kwenye pwani ya Tunisia, na kuna ongezeko la mzunguko wa majaribio ya kuvuka kwenda Ulaya kutoka Tunisia na Libya kuelekea Italia wakati hali ya hewa ikiwa imeimarika.