NA HAFSA GOLO
WAJASIRIAMALI Jimbo la Donge wametakiwa kutumia mbinu mbadala pamoja na ujuzi walionao kwa umakini ili waweze kuwa na soko endelevu la bidhaa wanazozalisha.
Mwakilishi wa jimbo la Donge, Dk. Khalid Salum Mohammed, alieleza hayo wakati alipokabidhi vyarahani vya kudarizi na vyengine vya kawaida kwa vikundi vinne vya wajasiriamali jimboni humo.
Alisema ni vyema kuhakikisha wajasiriamali hao wanatengeneza bidhaa zenye ubora ambazo zitakuwa ni moja ya kichocheo na kivutio kwa wateja mbali mbali.
Aidha alisema,baadhi ya watu wameweza kuondokana na umasikini sambamba na utegemezi ndani ya familia kupitia sekta binafsi ikiwemo kujiajiri wenyewe.
“Tujifunze kufanya kazi vizuri na kubadilishana uzoefu itasaidia kutimiza malengo tuliojiwekea”,alisema.
DK.Khalid aliwahakikishia wajasiriamali hao kuwa kutakuwa na utaratibu wa kupatiwa mafunzo endelevu ili waweze kubobea katika fani ya ushoni sambamba na kuingia katika ushindani wa kibiashara kutokana na ubora wa bidhaa watakazozalisha.
Aliwasisitiza kuzingatia umoja,upendo na mshikamano kwani ndio hatua muhimu itakayosaidia kutimiza ndoto zao.