NA TATU MAKAME

AKINAMAMA wanaofanya biashara za vyakula na kuuza matunda katika soko la Kinyasini, mkoa wa Kaskazini Unguja wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Wameeleza kuwa kiongozi huyo amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matatizo yanayowakabili wananchi wake na kuyafanyia kazi kwa vitendo.

Akinamama hao walitoa kauli hiyo Kinyasini kufuatia ziara maalum ya Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja kuangalia eneo linalojengwa soko la kudumu la akinamama wanaouza vyakula, matunda na kituo cha daladala kinyasini unaoenda sambamab na kurekebishiwa mtaro ambao ulikuwa  haupitishi maji.

Ziara ya Mkuu huyo imekuja kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.  Hussein Ali Mwinyi kufanya ziara mkoa huo na kutoa agizo kwa uongozi wa mkoa huo kuhakikisha unajenga soko la kudumu kwa akinamama wanaouza vyakula na matunda ili kuondokana na adha ya kufanya biashara eneo la wazi.

Walisema ziara ya Dk. Mwinyi, katika eneo hilo ni ishara tosha ya kutekeleza vyema ilani ya CCM pamoja na kukubali kwatumikia wananchi hivyo wananchi hao walimpongeza na kumtaka kuendelea vyema na majukumu yake ya kazi.

“Wakati Dk. Mwinyi alipokuja kuomba kura aliahidi mengi ambayo atayatekekeleza katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini leo hii tumeona dhamira yake ya kutumikia wananchi wake,” walisema wananchi hao.

Mfanyabiashara wa matunda Miza Othmani Nyange, alisema ziara ya Dk. Mwinyi ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani kwa vitendo hivyo alisema ziara hiyo ni moja ya sehemu ya majukumu yake ya kazi na kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.

Nae Aziza Saleh Ali ambae ni mfanyabiashara wa vyakula na lishe alisema kujengwa soko hilo kutaondosha usumbufu waliokuwa wakiupata wa kufanya biashara na kuendelea kufanya shuhuli zao sehemu za wazi baada ya banda walilokuwa wakitumia hapo wali kuangaku kwa upepo mienzi minne iliyopita.

“Furaha yetu imetimia leo kuja Rais kusikiliza kilio chetu na kujua shida zetu haijawahi kutokea, tunaendelea kumuombea shifaa na kumuungamkono kwa hali na mali ili atuongoze kwa salama,” alisema Aziza Saleh.

Mapema akitembelea eneo linalotarajiwa kujengwa soko na kukagua  ujenzi wa mtaro,   Ayoub alisema  ujenzi huo  utaanza  hivi  karibuni  na kuwataka wafanya biashara wa eneo hilo kuwa wastaamilivu katika kipindi cha ujenzi.

Ujenzi wa soko la kuuzia vyakula kwa  akina mama  wa soko  la  kinyasini unaojengwa  na  serikali  utasaidia kuondoa  malalamiko  ya wafanyabiashara hao wa kukosa sehemu za kufanyia  biashara  zao  kulikosababishwa  na  kuanguka  kwa mabanda kutokana  na upepo.