NAIROBI, KENYA

ZAIDI ya familia 450 zimeyakimbia makaazi yao katika eneo la Saku jimboni Marsabit nchini Kenya kutokana na hofu ya mapigano ya kikabila, kufuatia mauaji ya watu watatu waliopigwa risasi na majangili siku ya Jumatatu.

Nyumba kadhaa katika eneo la jirime kaatika sehemu ya bunge la saku jimboni Marsabit, zimekimbiwa na wenyeji kufuatia hofu ambayo inaendelea kushuhudiwa kutokana na uhasama wa kikabila.

Uhasama huo umeripotiwa kuzidishwa na kisa cha mauaji ya siku ya jumatatu ambapo watu watatu akiwemo mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa walipigwa risasi na kuawawa na watu wasiojulikana.

Naibu chifu wa jirime Adan Waqo ameeleza kwamba, huenda idadi yafamilia zilizoyakimbia makaazi yao  kutokana na hali hiyo ikawa ya juu zaidi kuliko taarifa walizonazo kwa sasa.

Idara ya polisi ya Marsabit imewataka wananchi kuwa na subra wakati uchunguzi ukiendelea na kuwasihi wenyeji kutohusika kwa kulipiza kisasi.

“Nawasihi wakaaji wa hapa wasijichukulie hatua mikononi mwao, Sisi kama idara ya polisi tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha wahalifu wanakamatwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Johnstone Wachira, mkuu wa polisi wa Marsabit Kati.

Mwakilishi wa wadi ya Marsabit ya Kati Hassan Jarso kwa upande wake, ameitaka wizara ya usalama wa ndani kuwajibika ili kupata suluhisho katika vita vya kikabila kama ilivyokuwa sehemu zingine za taifa.