NAIROBI, KENYA

WAKILI wa Nnamdi Kanu, anayeongoza kundi lililopigwa marufuku ambalo linataka kujitenga na jimbo la kusini mashariki mwa Nigeria, ameiambia BBC kwamba amekutana na mteja wake kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Alloy Ejimako amesema kiongozi wa watu wenye asili wa Biafra (Ipob) alionekana amedhoofika akiwa na alama za kujeruhiwa mikononi na kichwani.

Amesema Kanu ambaye anazuiliwa katika kituo kinachoendeshwa na polisi wa Nigeria wanaofanya huduma za siri, alimwambia alizuiliwa na kuteswa Kenya kabla ya kusafirishwa mwezi uliopita.

Kanu, ambaye anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na uhaini, alitoroka Nigeria mwaka 2017 akiwa nje kwa dhamana lakini alizuiliwa mwezi uliopita baada ya kukamatwa na kurejeshwa kutoka nchi ambayo mamlaka imekataa kuitaja.

Taarifa za vyombo vya usalama zinasema kuwa alikamatwa Kenya na kuzuiliwa kwa muda katika ubalozi Nigeria nchini kenya kwa wakati huo.

Wakili Ejimako anasema mteja wake amemfahamisha kuwa alizuiliwa katika kituo cha kibinafsi akiwa amefungwa nyororo kwenye sakafu ilikuwa na baridi kwa siku kadhaa.