NA MUHAMMED KHAMIS

AWAMU ya kwanza ya utekelezaji wa ugawaji wa mbegu kwa wakulima wa mradi wa viungo umezinduliwa jana kwa upande wa Unguja ambapo wakulima kutoka kanda ya Magharibi na Kaskazini Unguja wamegaiwa mbegu tofauti zikiwemo za vanilla, mboga na matunda.

Akizungumza katika ugawaji wa mbegu hizo meneja utekelezaji wa mradi wa viungo kanda ya Unguja, Khadija Ali Juma alisema mbegu hizo zimetolewa kwa lengo la kuendeleza kilimo kwa wakulima hao ambao walipatiwa mafunzo ya kilimo bora kupitia mradi huo.

Wakulima 238 walipatiwa mbegu hizo kwa hatua ya awali ambao ni miongoni mwa wakulima waliokwisha tayarisha mashamba yao kwa ajili ya kuanza shughuli za kilimo ikiwemo kupanda mbegu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Khadija aliwataka wanufaika  wengine wa mradi huo kuwa tayari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatayarisha mashamba yao ili waweze kuwa miongoni mwa wanufaika wa hatua za mwanzoni.

Akifafanua zaidi kuhusu ugawaji wa mbegu hizo kwa upande wa vanilla alisema jumla ya miche 2,700 imetolewa na kugawiwa kwa wakulima 27 ambapo kila mmoja atapata miche 100 kwa ajili ya kupanda kwenye shamba lake.

Katika hatua nyengine meneja huyo alisema kwa upande wa bustani za nyumbani (kitchen garden) hadi sasa wakulima 80 wamejitokeza na wapo tayari kuanza kilimo hicho na ametoa wito kwa wanawake wengine kujitokeza kwa wingi ili waweze kujifunza mbinu bora za kilimo hicho zitakazowasadia kupata lishe bora na kipato.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkulima wa vanilla kutoka kizimbani Unguja Haji Abdalla Abeid alishukuru mradi wa viungo na alisema utolewaji wa mbegu hizo kwao ni jambo muhimu na linalopaswa kupongezwa.

Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata wakati mgumu wanapohitaji mbegu za vanilla kutokana na gharama yake, lakini kupitia utekelezaji wa mradi wa viungo wameweza kupatiwa mbegu hizo bure bila ya gharama yoyote jambo ambalo limeongeza ari katika kuendeleza kilimo hicho.