NA HUSNA MOHAMMED
KESHO Zanzibar inatarajiwa kuanza kutoa chanjo ya ugonjwa wa kipindupindu katika baadhi ya maeneo ya Unguja na Pemba.
Utoaji huo wa chanjo ni moja ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa ukiisumbua sana Zanzibar kwa miongo kadhaa.
Karibu kila miongo ya mvua hasa zilizoongoka hapa Zanzibar ni kama ada lazima watu wauugue kipindupindu.
Hivyo kwa makusudi serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO) limeamua kudhibiti ugonjwa huo.
Zoezi hilo la chanjo litaendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza linatarajiwa kufanyika kuanzia kesho Julai 3 ikiwahusisha wananchi zaidi ya 327,000 wanaosihi katika shehia hatarishi za uwepo wa ugonjwa huo.
Maeneo hayo ni pamoja na Wiilaya ya mjini ambapo mitaa kama ya hauri moyo, Muembe makumbi, Chumbuni, Kwamtipura, Amani, Kilmahewa bondeni na Jan’gombe, huku Wilaya ya magharibi “B’’ Shehia ya Kinuni, Dimani, Mwanakwerekwe, Magogoni, Fuoni kibondeni, Tomondo na Meli nne watu watapewa chanjo hiyo.
Aidha maeneo mengine ni wilaya ya Magharibi “A” ambapo maeneo ya Mtopepo, Mwera, Mtoni, Bububu, Welezo na Mtoni kidatu, huku Wilaya ya Kaskazini “A” itahusisha Shehia ya Mkokotono, Kikobwweni na Banda maji, ambapo Wilaya ya Kaskazini “B” Shehia ya Mangapwani watu wake watapatiwa chanjo hiyo.
Pia Wilaya ya Kusini katika Shehia ya Kitogani na Muungoni, huku Wilaya ya Kati ikihusisha Shehia ya Ukongoroni.
Aidha zoezi hilo pia litatolewa katika kisiwa cha Pemba ambapo Wilaya ya Micheweni Shehia ya Kiuyu Mbuyuni, Maziwa n’gombe na Micheweni na Wilaya ya Wilaya ya Wete Shehia ya Kojani Mpambani na Kiuyu Minungwini.
Katika kulitekeleza zoezi hilo tunawanasihi wananchi walengwa wa maeneo tengefu ya chanjo kutoa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kukubali kupokea chanjo hiyo jambo ambalo litawaondoshea adha ya mara kwa mara kuugua kipindupindu.
Wananchi hawapaswi kuogopa kwa kuwa Chanjo hiyo ni ya kunywa na ina dozi mbili ambapo dozi ya kwanza inaanza leo huku dozi ya pili ikitolewa 31/7-4/8/2021.
Kwa mujibu wa wataalamu Chanjo ya kwanza hutoa kinga ya miezi 6 na unapokamilisha chanjo ya Pili basi utapata kinga ya miaka 3. Chanjo hii ya kipindupindu inahusisha watu wote waliofikisha umri wa mwaka 1 na kuendelea pamoja na Wazee na wenye magonjwa ya muda mrefu au kwa jina jengine magojwa sugu pia wanaweza kupata chanjo hii.
Wataalamu hao wanasema kuwa Chanjo hiyo ni salama na imethitishwa na shirika la afya Duniani (WHO) pia na Bodi ya chakula na vipodozi Zanzibar – ZFDA.
Sambamba na hilo, lakini Chanjo hii imeshawahi kutolewa katika nchi mbalimbali kama vile Ethiopia, Zambia, Msumbiji nakadhalika ambapo hadi sasa nchi hizo hazijaripoti matatizo yoyoye yanayohusiana na chanjo hizo.
Kwa vile hakuna ushahidi wa kutosha wakitaalamu juu ya usalama wa chanjo kwa mama wajawazito, hivyo basi wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja hawatapatiwa chanjo hii.
Historia ya kuwepo kwa maradhi ya Kipindupindu hapa Zanzibar inasemekana kwamba mripuko wa kwanza ulitokea katika robo ya mwisho ya karne 19, baadhi ya waandishi walieleza kwamba mripuko huo ulitokea katika mwaka 1888.
Katika mripuko huu ilikisiwa kwamba watu wengi (kwa maelfu), walifariki na walizikwa katika maeneo mbali mbali katika sehemu karibu na fukwe za bahari na katika maeneo ya Ng’ambo.
Mripuko mdogo ulitokea katika kisiwa cha Tumbatu mwanzoni mwa mwaka 1978 ambao uliwasibu wavuvi waliokwenda kuweka dago katika maeneo ya pwani ya Dar es Salaam.
Mripuko wa pili mkubwa ulitokea Mjini Unguja hapo Machi, 1978, ambapo watu wengi waliathirika na ugonjwa ulienea hadi katika baadhi ya mashamba yaliyo karibu na Mjini.
Maeneo kama Saateni, Amani; Viwanda Vidogo Vidogo kwa njia ya kuelekea upande wa mashariki, Magomeni “Round About” barabara inayoelekea Kusini na
Aidha historia inaonesha kuwa Miripuko 19 tangu kipindi hicho imeshatokezea hapa Zanzibar, ambapo zaidi ya wagonjwa 14,364 wameuguwa kipindupindu na vifo 210 vimeripotiwa kutokana na maradhi hayo.
Miripuko hiyo imekuwa ikitokezea wakati au mara tu baada ya msimu wa mvua kubwa, hasa za Masika na Vuli za kila mwaka.
Takwimu zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba miripuko mingine midogo midogo ya maradhi haya imekuwa ikitokezea kila mwaka katika nchi au maeneo tafauti.
Inakaridiwa kwamba mirupuko hii imekuwa ikiathiri kati ya watu milioni 1.3 hadi milioni 4 kila mwaka, na husababisha vifo vya watu kati ya 21,000 hadi 143,000 kila mwaka.
Kimsingi ugonjwa wa kipindupindu umebainika kujitokeza mara kwa mara hapa nchini mara baada ya kumalizika kwa mvua za msimu ikiwemo Vuli na Masika, hivyo kuleta athari kubwa kwa jamii ikiwemo vifo.
Moja wapo kati ya magonjwa yanayohusishwa na uchafu wa kupindukia ni ugonjwa wa Kipindupindu ambao unaripotiwa kwua ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri sana jamii hasa katika nchi zinazoendelea.
Hatua hiyo imeipelekea Shirika la Afya Duniani (WHO), limeuweka ugonjwa huu kama mojawapo ya viashiria vya maendeleo ya jamii husika ambapo shirika hilo limeona ipo haja ya kutoa chanjo hiyo hapa Zanzibar kutokana na historia ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huu hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binaadamu uletwao na vimelea vya bacteria vijulikanavyo kitaalamu kama Vibrio Cholerae.
Kwa kawaida vimelea hawa hupendelea kuishi katika kinyesi cha binaadamu ambapo mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hivi vya kipindupindu.
Mara baada ya kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa, baadhi ya vimelea huuwawa kwa tindikali iliyokwenye tumbo pindi chakula au maji haya yanapoingia tumboni lakini hata hivyo baadhi ya vimelea hawa hufanikiwa kukwepa ukali wa tindikali hii na hivyo kuendelea kuishi.
Hivyo tuwape ushirikiano watendaji wa wizara ya afya na kukubali kupokea chanjo, ili kuona ugonjwa wa kipindupindu unakuwa historia Zanzibar.