WAPENZI wasomaji wetu leo tunaendelea tena na safu yetu ya mapishi ambapo nimewatayarishia upishi pambe wa Wali Wa Kichina Wa Kuku Na Mboga mchanganyiko.
Ikiwa tuko katika kumalizia sikukuu ya eid el Hajj na leo mwisho wa wiki ni vyema familia ikapika upishi huu mzuri kusudi kuburudika katika upishi wa mchana.
Ili kuupika upishi huu ni lazima kuwa na mahitaji haya yafuatayo:-
VIPIMO
Mchele wa basmati/pishori – 4 vikombe vikubwa (mugs)
Kuku – 2
Vitnguu vya kijani (sprin onions) katakata – 5 miche
Maharage machanga (spring beans) katakata – kiasi kujaza mug moja
Pilipili boga la (capsicum) katakata – 1
Karoti katakata vipande virefu – 1
Kitunguu thomu (garlic) kuna (grate) – 1 kubwa
Tangawizi mbichi kuna (grate) – 1 kubwa
Sosi ya soya (soy sauce) – 2 vijiko vya supu
Kidonge cha supu – 1
Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe cha chai
Chumvi – kiasi
Pilipili manga – 1 kijiko cha supu
NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA
- Osha kuku vizuri, katakata vipande, weka katika sufuria, tia chumvi, pilipili manga, mfunike, umkaushe motoni huku ukimgeuza geuza.
- Roweka mchele kisha uchemshe uive nusu. Chuja maji, tia siagi kidogo ili usigandane.
- Weka karai ya kupika mboga (wok) au sufuria kisha tia mafuta yashite moto.
- Tia kitunguu thomu, tangawizi, kaanga kidogo.
- Tia mboga zote, ulizokatakata.
- kaanga kidogo, kisha tia sosi ya soya na kidonge cha supu. Usizipike sana mboga mpaka zikalainika mno. Sababu zitaiva katika mchele
- Changanya kuku na mboga kisha changanya vyote katika mchele, urudishe katika moto.
- Funika upike hadi uive kamilifu.
- Pakua kwenye sahani.
Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)