NA ASYA HASSAN

ZAIDI ya walimu 88 kutoka skuli mbalimbali za Unguja na Pemba wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya kuogelea na uokozi ili waweze kuwafundisha wanafunzi wao.

Mafunzo hayo yanayotolewa na taasisi ya Panje Project, yameelezwa kuwa yatawasaidia walimu hao kuwafundisha wanafunzi wa skuli na kuisaidia jamii pale panapotokea matatizo ya baharini ikiwemo kuzama.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kikwajuni wilaya ya Mjini Unguja, Meneja wa taasisi hiyo, Muhammad Suleiman Said, alisema wanatoa mafunzo hayo ikiwa ni mwendelezo kwa taasisi hiyo kutoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ya watu.

Meneja huyo, alifahamisha kwamba mafunzo hayo yatawashirikisha walimu wa skuli za sekondari hivyo kupitia mafunzo hayo itakuwa chachu kwa wizara ya elimu kuweza kurithi somo hilo kuanza kusomeshwa maskuli.

Meneja huyo alisema kufundishwa kwa walimu hao itakuwa chachu kwa somo hilo kusomeshwa watoto wa skuli kutokana na watoto hao ni rahisi kukamata mafunzo na kuweza kuleta tija pana hapo badae.

“Ni kawaida kwa taasisi ya Panje Project, kutoa mafunzo hayo kwa makundi tofauti kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kuweza kuhimili matukio ya ajali pale zinapotokea,”alisema.