NEW DELHI, INDIA
IDADI ya watu waliopoteza maisha kwa janga la mafuriko katika jimbo la Maharashtra nchini India imefikia 149 huku makumi ya watu wakiwa bado hawajulikani walipo.
Mamlaka husika katika jimbo hilo la Maharashrat la magharibi mwa India zinasema kuwa, juhudi za kuwatafuta watu waliopotea zinaendelea ingawa matumaini ya kuwapata hai yanazidi kufifia hasa baada ya kupita siku kadhaa tangu wapotee na kuna uwezekano wakawa wamesombwa na maji au kufikiwa na udongo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, timu za uokozi zinaendelea na kazi zao zikishirikiana na jeshi la India huku tathmini ya maafa ya mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku chache zilizopita katika jimbo hilo ikionyesha ukubwa wa janga hilo.
Wakati huo huo, mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu yaliendelea kutoa misaada ya chakula, dawa na nguo kwa waathirika wa mafuriko hayo huku ikielezwa kuwa, watu karibu 230,000 waliokolewa kutoka katika maeneo waliokuwa wamekwama baada ya nyumba na makaazi yao kusombwa na maji.
Mbali na Maharashtra, baadhi ya majimbo mengine yaliyokumbwa na mafuriko ya hivi karibuni nchini India ni Kerala, Karnataka, Assam na Odisha.
Janga hilo la mafuriko na maporomoko limeteketeza mamia ya vijiji baada ya kusomba nyumba na kuwaacha raia wa maeneo hayo bila makaazi.
Baadhi ya maeneo ni vigumu kuyafikia kutokana na kukatika kabisa mawasiliano ya barabara baada ya madaraja kubomoka huku mawasiliano ya simu katika maeneo hayo yakikatika.