WALIOFIKIRIA kuzireshesha tena mbio ndefu za kimataifa za marathoni hapa Zanzibar, kwa hakika wamefanya jambo la maana sana, kwani mbio hizo kama zitaandaliwa vyema zina mchango mkubwa kwenye sekta kiongozi ya uchumi wetu ambayo ni utalii.
Mbio za marathoni za Zanzibar awali zilikuwepo, badaae zikapotea kwa takriban kipindi cha miaka 18, kwa hakika tuchukue nafasi hii tunawapongeza wale waliofikiria kuzirejesha tena kwani kwa hakika kama vile wameuamsha kwenye usingizi mzito.
Kwa ujumla wake Zanzibar tuna sifa ya kuwa wa mwanzo kubuni na kuanzisha vitu vizuri vyenye manufaa makubwa kwa nchi, hata hivyo tatizo letu lipo katika kuviendeleza vitu hivyo kwa kisingizo cha kudumu kinachoitwa ‘kutokuwa na fedha’.
Kuna mifano mingi, lakini tunaweza kujiuliza kwanini mbio za kimataifa za marathoni na trithoni ziliozokuwa zikifanyika kila mwaka hapa visiwani na kuvutia mashabiki kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni zimepotea kwa takriban miaka 18?
Bila shaka jibu la haraka ni lile lile ‘kutokuwa na fedha’ za kuendesha mashindano hayo. Mipango yetu mingi tunashindwa kuitekeleza na kueindeleza kwa sababu ya kutokuwa na fedha hasa kwa kutegemea bajeti serikalini.
Tunakubali serikali inao mchango wa kuwa na bajeti ya kuendesha mashindano ya marathoni na triothoni, lakini kutoka na wingi wa majukumu ya wananchi hulazimisha kuhaulisha fedha hapa na kupeleka pengine.
Sisi tunaamini hicho hakikuwa kigezo kabisa cha kusitishwa michuano hiyo kwani kama mipango endelevu ingekuwepo ya kuhakikisha mbio hizo zinadumu katika ardhi ya Zanzibar, tusingefikia hatua ya kupotea kwa muda wote huo.
Hatukatai ni kweli ipo mipango utekelezwaji wake lazima uwe na bajeti serikalini, lakini kwa mbio za marathoni na trithoni zilizokuwa zikifanyika Zanzibar zingeweza kuendeshwa bila ya kutegemea bajeti ya serikali.
Kama tungeacha kidogo uvivu wa kufikiri bila shaka tungebaini hakuna sababu kwanini wafanyabishara na wawekezaji waliopo Zanzibar hasa kwenye sekta ya utalii washindwe kuchangia uendeshwaji wa mbio hizo.
Mbio za marathoni tunazozizungumzia za miaka ile zilizokufa zilikuwa za kimataifa kweli, kwani wakimbiaji walitoka sehemu mbalimbali. Wapo waliotoka Ulaya, wapo waliotoka Afrika na sehemu nyengine.
Zanzibar tuna miradi mingi ya uwekezaji hasa kwenye utalii hivi kama tungezishawishi na kuzieleza faida watakazozipata hoteli kubwa zenye nyota tano kuchangia mayatarisho ya mbio hizo zingeshindwa kweli?