LAGOS, NIGERIA

KUNDI la wanamgambo wenye silaha limeshambulia mji wa Faru wa kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua kwa watu 45 na kuwajeruhi makumi ya wengine.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na duru hospitali pamoja na wakazi wa eneo hilo. Shambulio hilo la kigaidi lilitokea jana katika mji wa Faru ambapo lilizua mtafuruku na wahaka mkubwa hasa baada ya kutokea mauaji hayo ya kutisha.

Abubakar Ilyasu mmoja wa wakazi wa mji huo alisema, takribani wanamgambo 100 waliokuwa wamepanda pikipiki waliuvamia mji huo na kuanza kufanya mauaji kwa kuwamiminia risasi watu wasio na hatia yoyote.

Hujuma, mauaji na utekaji nyara wa umati wa wanafunzi na baadaye kudai kikomboleo, yamegeuka na kuwa jambo la kawaida kabisa kaskazini magharibi mwa Nigeria huku vyombo vya usalama vikilaumiwa kwa kushindwa kuwalinda raia.

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa kundi la Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS

Hujuma na mashambulio ya Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.

Mwezi uliopita wa Juni Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alikiri kushindwa kuwamaliza magaidi wa kundi la Boko Haram na kuwaletea amani wananchi wa nchi hiyo.

Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Buhari inakosolewa vikali kieneo na kimataifa kwa kushindwa kukabiliana na wanamgambo magaidi wa Boko Haram, huku wachambuzi wa mambo wajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kuhusiana na  vitendo vya mara kwa mara vya utekaji nyara mamia ya wanafunzi.