NA MWANDISHI WETU

TAKRIBAN siku tatu sasa tangu kuanza kwa mfumo mpya wa tozo kwa wale wanaotumia simu za mkononi kufanya miamala ya fedha yaani kutuma na kupokea umeanza kutumika hapa nchini Tanzania.

Kufuatia hali hiyo, wananchi wengi wanaotumia mfumo huo wameonekana kuwa na hofu kubwa juu ya tozo kutokana na gharama zake kuonekana kuwa mzigo kwa wananchi na hasa wakati ambako kunashuhudiwa kupanda kwa gharama nyingine za maisha kulikosababishwa na ongezeko la kodi katika nishati ya mafuta ya diesel na petrol.

Kwa mfano kwa kuangalia ukokotoaji wa tozo hizo, mtu aliyekuwa akipokea fedha kiasi cha shilingi 100,000 kutoka kwa wakala alikuwa akikatwa kiasi cha 3,600, sasa atakuwa akikatwa jumla ya shilingi 6,100 na kiwango hicho kinazidi kupanda kadri muamala wa fedha unavyoongezeka.

Lakini jambo linaloonekana kuwaumiza wananchi zaidi ni lile la makato hayo kufanyika zaidi ya mara mbili, yaani mtumaji na mtumiwaji. Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa imezoeleka hapo nyuma wakati ambapo makato ya fedha yaliyokuwa yakifanyika kwa mpokeaji wa fedha pekee lakini sasa tuzo hiyo inakula pande zote mbili.

Tozo hizo zinaonekana kuwazidisha wasiwasi kwa wananchi wanaohofia siyo tu uwezekano wa kupanda kwa gharama za maisha bali pengine kuanguka katika shughuli zao kutokana kuwabana watu wa kipato cha aina yoyote huku ikizingatiwa kuwa baadhi ndio kazi yao inayowapatia riziki ya halali.

Licha ya kilio cha wengi, Serikali inaonekana kukaza kamba ikisistiza kuwa hakuna namna nyingine  mbali ya tozo hiyo iliyoanza Julai 15 na kuendelea.

Hatua hiyo ya serikali siyo tu inaacha hofu kwa watumiaji wa huduma za simu za mikoni lakini pia inaibua wasiwasi mwingine juu ya majaliwa ya mitandao hiyo kuendelea na kushamiri huku wengi wakihofu kuwa pengine watumiaji wakatafuta njia nyingine mbadala kama vile huduma za kibenki.

Hivi karibuni kiwango cha matumizi ya simu za mikononi kimekuwa kikiongezeka na ongezeko hilo linashuhudiwa pia katika maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme imeanza kuimarika.

Kuwepo kwa kodi hiyo pengine kukawa ni pigo kubwa kwa wananchi hao wa vijijini ambako huduma za simu za mikononi kwao siyo jambo la anasa bali ni nyenzo muhumu inayotumika kuendesha maisha kama vile kusaka masoko ya mazao yao.

Pamoja na mambo mengine wananchi wanatakiwa kuizoea hali hiyo kwa kuwa nchi za wenzetu hata kitu kidogo unalipia kodi jambo ambalo hata huku kwetu Tanzania linawezekana kabisa kama ulivyo mfumo huo mpya.

Kwa mfano Ripoti ya hali ya uchumi Tanzania toleo la Juni 2020 kutoka Benki ya Dunia (WB) inaonesha ni asilimia 23.4 tu ya watu kwenye sehemu za mijini wenye akaunti za benki, na asilimia 5.1  ya watu vijijini wana akaunti za benki.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba namna pekee Watanzania wengi hujumuishwa katika huduma za kifedha ni kupitia huduma za kifedha za simu (mfano, M-Pesa, Tigopesa, Halopesa na zinginezo).

Huduma hizi zimeendelea kuwa na watumiaji wengi ambapo mpaka kufikia Aprili 2021 kulikua na watumiaji  milioni 32 wa huduma za fedha kwa njia ya simu. Hata hivyo, idadi hii bado hailingani na idadi ya watumiaji wote wa simu ambapo mpaka Aprili 2021, kulikua na watumiaji milioni  53.

Moja ya sababu kubwa inayotajwa za watu kutokutumia huduma ya kutuma fedha kwa simu kwa uwezo uliopo, ni gharama katika kutumia huduma hizo, hususani kwa miamala midogo midogo inayotumiwa na watu wengi.

Katika nyakati hizi ambazo watu wanahitaji kuwasiliana zaidi, kazi nyingi zinafanyikia kwenye mtandao, kuongeza tozo tena juu ya gharama za mawasiliano ni mambo mawili ama kuimarisha uchumi wa Tanzania au kuwaumiza hasa wananchi wa chini.