NA MWANDISHI WETU

LICHA ya kuwepo kwa wimbi la kesi za ubakaji na talaka hapa Zanzibar, lakini imebainika kuwa kesi zinazoongoza ni zile zinazotokana na migogoro ya ardhi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba hasa sehemu za vijijini.

Daima migogoro inayotokana na ardhi imekuwa ikilalamikiwa nah ii inatokana na ukiukwaji mikubwa wa sheria za ardhi kiasi kwamba Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amelikemea katika ziara zake alizofanya hapo juzi Mkoa wa Kusini Unguja.

Wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika mkoa huo, alisema kuwa  licha ya kuwepo Sheria zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi hapa Zanzibar lakini bado watu hawaziheshimu na hawazifuati.

Kwa mfano sheria ya Matumizi ya Ardhi Namba 12 ya mwaka 1992, Sheria ya Uhaulishaji wa Ardhi Namba 8 ya mwaka 1994 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi Namba 7 ya mwaka 1994 ambayo ndiyo inayohusiana na uanzishwaji wa Mahakama ya Ardhi nis heria nzuri lakini utekelezaji wake bado ni mdogo.

Ni ukweli usiopingika kuwa ardhi yetu ya Zanzibar ni ndogo hivyo kutotumika vizuri kwa kiasi kikubwa inaweza kuleta matatizo hapo baadae.

Kwa mukhtaza huo bila ya kumung’unya maneno, kwa bahati mbaya wavunjaji wa sheria hizo ni baadhi ya viongozi ama watendaji wa Serikali na matukio mengine yanayofanywa na wananchi wa kawaida ambapo kwa baadhi yao wamekuwa wakichangia migogoro ya uvamizi wa maeneo ya Serikali, wananchi na wawekezaji na mingine kadhaa.

Kwa kweli hali hii haipendezi kabisa kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu wamekuwa wakinyang’anywa kwa makusudi rasilimali ya ardhi ilhali ana nyaraka zote muhimu za umiliki wa ardhi na kupewa wasiostahiki tena kwa makusudi.

Tunaamini kuwa unaweza kufika wakati rasilimali hiyo ya mchanga inaweza kukosekana kabisa kama hakutafuatwa sheria ama kuweko mpangilio mzuri jamboa mbalo ni hatari hasa kwa kizazi kijacho.

Jumla ya kesi 207 za migogoro ya ardhi Zanzibar zilifunguliwa kuanzia Julai 2015 hadi April 2016 mwaka huo na hii ni ile ambayo inaripotiwa kwani kuna baadhi ya watu hushukuru kimya kimya.

Inafahamika wazi kuwa miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa zikizidisha mrundikano wa kesi hizo ni pamoja na ucheleweshwaji wa kesi ambao husababishwa na mawakili ambao ni wachache katika mahakama hizo.

Katika maelezo yake alisema kamwe uongozi wa awamu ya nane ulioko  madarakani ni lazima kuhakikisha unafuatilia kwa karibu katika kutatua migogoro ya ardhi na haitokuwa tayari kuibua migogoro mipya na kuutaka uongozi huo kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto za ardhi zilizopo.