KWA zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa dunia inakabiliwa na kitahanani cha janga la ugonjwa wa corona, ambapo kwa kiasi kikubwa gonjwa hilo limeathiri sekta zote zikiwemo za kijamii, kiuchumi na kubadilisha mfumo mzima wa maisha.
Ugonjwa huo kwa mara ya kwanza uligunduliwa katika mji wa Wuhan uliopo China mwezi Disemba mwaka 2019, ukasambaa kwa kasi kubwa kwani ndani ya miezi sita corona ilifika kila pembe na kona ya dunia.
Hivi tunavyozungumza janga la maradhi hayo limeshapoteza zaidi ya watu milioni 4 na watu zaidi ya milioni 194 wamepata maambukizi duniani kote, ambapo nchi mbalimbali ikiwemo Zanzibar zinaendeleza mikakati ya kudhibiti maambukizi zaidi.
Wataalamu wa sayansi za afya kwa upande wao hawakupakata mikono wakishuhudia maambukizi zaidi na vifo vikiongezeka duniani, bali waliingia maabara angalau kutafuta chanjo kwa haraka kama wameshindwa kuipata dawa ya corona.
Hatimaye kupitia wataalamu hao kampuni kutoka nchi mbalimbali zimefanikiwa kugundua chanjo za kuudhibiti ugonjwa wa corona, ambapo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), zimeidhinisha matumizi ya baadhi ya chanjo hizo.
Kwa kawaida WHO kabla ya kuidhinisha matumizi ya dawa ama chanjo kwa matibabu ya mwanadamu, lazima wazifanyie uhakiki wa kina juu ya usalama na ulinzi wa maisha ya mwanadamu ambaye ndiye mlengwa wa matumizi.
Kwenye suala la chanjo ya corona, WHO haikukurupuka kuidhinisha matumizi ya chanjo hizo, bali ilizipitisha kwenye hatua mbalimbali kuangalia usalama wa maisha ya watumiaji na baadae kubaini kuwa zipo salama na hazina madhara.
Kinachotushangaza ni kuibuka kwa kasumba zinazoendelea kusambazwa mitaani zisizo na msingi zinazolenga kupotosha usalama wa afya kwa watumiaji wa chanjo hizo.
Kwa mfano wapo wanaodai kuwa endapo utapatiwa chanjo hizo baada ya miaka miwili unaweza kufariki dunia, wapo wnegine wanadai kuwa chanjo hizo zinaletwa kuja kumaliza kizazi hasa miongoni mwa waafrika.
Hatuelewi wasambaza kasumba hizi wanalengo gani kwani kwa tunavyoelewa kasumba hizo na nyenginezo zote zinalenga kuitia hofu jamii isijitokeze kupewa chanjo ya corona na hivyo kuongezeka kasi ya maambukizi.