NA HAJI NASSOR
WAFUNGWA wanaotumikia vifungo katika vyuo vya mafunzo kisiwani hapa, wameiomba mahakama kuu kuharakisha kupelekwa Jaji mkaazi, ili kesi za mahakama kuu zisikilizwe haraka.
Walisema hao mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, aliefanya ziara ya kutembelea vyuo vya mafunzo ikiwa utaratibu aliojipangia kila mwaka kutembelea mahakama na vyuo vya mafunzo Unguja na Pemba.
Walisema kutokuwepo Jaji mkazi kunasababisha kesi zinazohusiana na mahakama kuu kuchelewa kutolewa uamuzi.
Aidha, wameiomba serikali kufikiria uwezekano kwa dhamana zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwahusisha pia wafungwa kutoka Zanzibar.
Walisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja, hivyo hawaoni sababu ya msamaha wa Rais kuwanufaisha wafungwa wa upande mmoja.
“Mifumo wa mahakama ni tofauti kati ya Zanzibar na Tanzania Bara lakini kunaweza kuandaliwa utaratibu wa wafungwa kutoka Zanzibar pia kunufaika na msamaha huo,” walisema.
Walimueleza Jaji Mkuu kuwa ili kuimarisha muungano ulioasisiwa mwaka 1964, ni vyema kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anapotoa msahama kuwafikia na wafungwa walioko Zanzibar.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mohamed Salim Mohamed, anayetumikia adhabu ya kupatikana na dawa za kulevya, alisema ni vyema suala hilo kuangaliwa.
“Tunaskia kuwa hivi karibuni wakati tunasherehekea miaka 57 ya Muungano, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwapa msahama wafungwa zaidi ya 5,000, lakini Zanzibar hakuna hata mmoja, wakati huyu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.