NA ASYA HASSAN

WAJASIRIAMALI wanaofanya shughuli za kuanika dagaa katika shehia ya Mangapwani, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Unguja, wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwawekea miundombinu mizuri ya kupatikana huduma zote za kijamii.

Walitoa kilio hicho mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum, hivi karibu alipofika katika maeneo hayo kuangalia mazingira ya ufanyaji shughuli hizo.

Walisema mazingira ya ufanyaji wa shughuli hizo hauridhishi kwa sababu hakuna miundombinu ya upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, vyoo , barabara na eneo la kuanikia madagaa.

Walisema hali hiyo haileti taswira nzuri na hairidhishi kwani husababisha uchafuzi wa mazingira pamoja na kuhatarisha afya zao na watu wengine wanaofika katika eneo hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Sambamba na hayo wajasiriamali hao walisema ni vyema serikali kukaa na kuliangalia suala hilo kwa upana wake kwani wao wamejiajiri katika eneo hilo ili kuongeza kipato chao na kuongeza mapato serikalini.

Walisema malalamiko hayo tayari washayafikisha serikali ya wilaya ya Kaskazini ‘B’ pamoja na Baraza la Manispaa la wilaya hiyo lakini bado hadi leo changamoto hizo hazijapatiwa ufumbuzi.

“Hapa kila mwezi fedha za kodi zinakusanywa na changamoto zetu wanazijua lakini bado hakuna kitu hata kimoja kilichoweza kupatiwa ufumbuzi hadi sasa hivyo kupitia kwako Waziri mategemeo yetu unaweza kutusaidia,” walisema.

Naye Waziri Saada alisema serikali itaendelea kuboresha huduma za wananchi pamoja na kutoa miongozo kupitia maeneo tofauti ikiwemo ya biashara na huduma nyengine ili kuondosha changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi na kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Alisema serikali imekuwa ikisisitiza wananchi kujiajiri ili kuongeza kipato chao na taifa kwa ujumla hivyo watahakikisha changamoto zilizopo katika eneo hilo zinapatiwa ufumbuzi kadri ya serikali itakavyojipanga.

Akizungumzia suala la mazingira waziri huyo alisema atakaa na watendaji wake ili kuona mazingira ya eneo hilo yanaimarishwa ili wafanyabiashara hao waweze kufanya shughuli zao katika hali ya usalama.