Wataka usaidizi kufikia zaidi malengo yao

HABIBA ZARALI, PEMBA

“SIKUTAKA kujiingiza kwenye tabia ya omba omba kwa sababu ya ulemavu wangu wa uoni, bali napambana na kujitafutia rikizi kila siku,” anasema Ali Hemed Khalifa Mwenyekiti wa Ushirika wa Wasioona Mtambile.

Akiwa na wanachama wa ushirika huo mwenyekiti huyo na wenzake hutengeneza bidhaa mbalimbali ambapo anasema kwa kazi hiyo, licha ya kuwa wao hawaoni lakini hawalali na njaa.

Ali Hemed Khalifa, ndiye muanzilishi wa ushirika huo wa wasioona, ambapo alinisimulia mengi yanayohusu ushirika wao pamoja na wasioona wanavyoweza kuleta mabadiliko.

Mwenyekiti huyo anasema wao wanaendesha kazi zao za kushona bidhaa zinazotokana na usumba, na kutengeneza sabuni na kisha mkono wao kwenda kinywani.

Anasema kikundi hicho chenye watu tisa,wanawake saba na wanaume wawili, kabla ya hapo hawakuwa na kazi yoyote ya kufanya na kilichokuwa kikiwatawala ni unyonge wa maisha yao.

Mungu haachi mjawe, aso hili ana lile, lakini Mungu hakupi kilema ukakukosesha mwendo misemo hiyo yote imesibu katika kikundi hiki cha wasioona kilichopo Mtambile wanaofanya kazi zao kwa ubora na umahiri mkubwa.

Ali hemed alisema kuwa ushirika wao, ulianza rasmi mwaka 2001, baada ya kupata mafunzo kupitia ufadhili wa Abilis Foundation kutoka Finland, iliyoko Unguja ambapo walijifunza kutengeneza mazulia na madometi ya usumba na baadaye sabuni.

“Nialipoaanza safari ya kuwasaka wasioona wenzangu mmoja baada ya mwengine, kwa kila eneo analoishi mwanachama wa Jumuia ya Wasioona Wilaya ya Mkoani, mimi napata mshangao sana kumuona mtu mwenye ulemavu anakuwa mnyonge wa maisha yake wakati kumbe kila mmoja anaweza kufanya kazi kutokana na hali yake na akaweza kujikimu kimaisha”, anasema huku akiendelea na kazi ya kutengeneza dometi.

Kazi yao hiyo imeweza kuwaingizia kipato kwenye familia zao na hata maisha yao binafsi kwa kujikimu mahitaji yao ikiwa ni pamoja na chakula, kusomesha watoto, kujinunulia nguo na hata kuacha utegemezi waliokuwa nao.

Kabla ya kupata ujuzi huo, walikuwa wanategemea kutoka kwa jamaa zao wa karibu jambo ambalo lilikuwa linawakwaza katika mfumo mzima wa maisha yao kwani wasipogaiwa hawakumiliki kitu.

Walisema kuwa dometi moja hulitengeneza kati ya siku mbili hadi tatu, ambapo moja huliuza kati ya shilingi 20,000 na shilingi 25,000.

“Kukaa tu nyumbani bila ya kazi ya kufanya huwezi kuwa na maisha mazuri mtu yoyote hapaswi kudharauliwa unaona sisi wasioona tunajikimu kwa kufanya kazi za mikono,” anasema.

Akimtolea mfano mwanachama wa kikundi hicho Mkasi Simai Makame, ambae alikuwa hajawahi kutoka nje tangu  azaliwe zaidi ya miaka 20, na baada ya kufika kwa wazazi wake kumuhitaji kujiunga katika kikundi hicho walikuwa hawataki kumtoa kwa kumuona hatoweza kwa kutoona kwake.

“Juhudi kubwa ilifanyika, hadi mwanachama huyo kuweza kuingia kwenye ushirika huo, na wazazi wake kuridhia ingawa kwa hapo awali, ni kwa shingo upande”, alisema.

Ali alisema awali ushirika huo ulikumbwa na changamoto kadhaa, uliendelea kwa kuchangishana fedha kila mwanachama shilingi 5,000 kwa ajili ya kununulia malighafi ya usumba, ingawa baadhi yao walikuwa wagumu kutoa wakidhani wanataka kuibiwa ila baadae walikubali na kupata fedha za kununulia malighafi.

Alifahamisha kuwa pamoja na uhaba wa mtaji, lakini kwa sasa tayari wanachama wote wa ushirika huo, wameshapata uelewa wa kutengeneza madometi na mazulia, ambapo pia hujipatia fedha ndogo ndogo ya sabuni na ya kujikimu kwa chakula na hata mavazi.

“Mimi nilijua kutokana na ulemavu wangu wa uoni, siwezi kufanya lolote, lakini kwa sasa naweza kufanya makubwa, maana hata sabuni yangu hainipigi chenga,’’ alisema wakati akitengeneza zulia.

“Wazazi wa mkasi wakizungumza na makala haya alisema hawakufikiria kama mtoto wao angeweza kuwa na ujuzi unaoweza kumuingizia kipato kutokana na ulemavu wake hasa pale alipofikia hatua ya kujiajiri mwenyewe kwa kuanzisha mpango wa kujishonea mikoba, makawa na mikeka jambo ambalo hapo awali hawakulitarajia”, alisema.

Nae Bi Tumu ambae ni mmoja wa wanachama hao anasema baada ya kufika ndani ya ushirika huo, pia ameweza kujionea faida ya kufanya kazi hasa pale anapoona anaingiza kipato.

“Kwa kweli ushirika huu, umeniwezesha kuyatawala mazingira yangu, na hata kujidai kwa kupata angalau sabuni, kanga na vijora na hata kusaidia wenzangu,”anasema.

Naye mwanachama, Riziki Juma Omar, anasema iwapo ushirika wao utasaidiwa na wafadhili, unaweza kupiga hatua kubwa zaidi, na wasiiona katika ukanda huo wa Mtambile.

Kubwa zaidi wanachama wa ushirika huo, pamoja na kulilia mtaji, lakini pia wamepaza sauti zao juu, kutaka kupatiwa mafunzo zaidi ya kazi yao hiyo, ili waingie katika soko la ushindani.

“Changamoto kubwa kwa sasa ni malighafi ambayo baadhi ya siku inamlazimu mwenyekiti wetu asafiri hadi kijiji cha Bumbwini Unguja au Kaskazini Pemba, kuyafuata makumbi au Kamba”, alisema mmoja wa wanaushirika huo.

“Bidhaa zetu tunauza maofisini, mahotelini, mitaani na katika soko la Jumapili liliopo mjini Chake chake, ingawa nalo lishaanza kupoteza uhalisia wake,” aliongeza.

Hata hivyo wanachama hao wametoa wito kwa wazazi na walezi, kuacha tabia ya kuwafungia ndani watu wenye ulemavu, kwani wakiwezeshwa kwa mujibu mazingira yao, wanaweza kuleta mabadiliko.

Pia waliiomba serikali kuwasaidia, ili waweze kujikongoja na kufikia malengo yaliojipangia, ikiwa ni pamoja na kukuza pato lao.

Ushirika huu ambao, unajiendesha kwa nguvu za wanachama wamekuwa na utaratibu wa kugawana shilingi 20,000 kila baada ya kuuza mazulia na fedha nyengine kununua malighafi.

Nae mratibu wa mafunzo ya ‘Usumba Project’ waliyopata wanaushirika huo kupitia ufadhili wa Abilis Foundation kutoka Finland, Massoud Suleiman Daudi anasema kupatiwa mafunzo hayo kwa wasioona ni kuwawezesha, ili kuondokana na utegemezi kwani nao ni sawa na wengine.

“Muhimu ni kuwapa mafunzo na mwamko wa kujitambua, wasionekane kama ni wenye ulemavu kabakia nyuma nyuma wawezeshwe nao kama wanavowezeshwa wengine,” alisema.

Mratibu wa Idara ya watu wenye Ulemavu Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, alisema wamekuwa wakiwasaidia watu wenye ulemavu hasa kupitia vikundi vyao, kila hali ya fedha inaporuhusu.

“Unajua kwa sasa watu wenye ulemavu wamehamasika na kuanzisha vikundi vyao, sasa serikali imekuwa ikiwasaidia kwa awamu, lakini pia ni nafasi ya wafadhili nao kuwasaidia,” anasema.

Zanzibar ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012, inajumla ya watu milioni 1.303 kati ya hao wanaume wakiwa 630,677 na wanawake 672,892. Kati ya hao wenye ulemavu ni 8,343. Miongoni mwa wenye ulemavu hao, wanaume ni 4,380 na wanawake ni 3,963.

Sheria ya Watu wenye ulemavu, haki na fursa nambari 9 ya mwaka 2006, kifungu ch 5 kimebainisha kuwa pamoja na serikali kuchukua hatua za hali ya juu kadiri ya rasilimali iliyopo ili kuwawezesha watu wenye ulemavu.

Kifungu hicho kikafafanua kuwa, viwango vilivyowekwa katika sheria hii ni viwango vya chini vya wajibu wa kisheria vya utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu na bila ya kuathiri haki za watu wenye ulemavu.

Lakini Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu ibara ya 5, imetambua usawa na kutobaguliwa kwa watu wenye ulemavu katika mazingira yoyote yale.

CAP

BAADHI ya wanaushirika wa walemavu wasioona kisiwani Pemba wakiwa katika moja ya kazi yao ya kusokota Kamba ya usumba kwa ajili ya kutengenezea madometi kama walinyokutwa huko ofisini kwao Mtambile Mkoani Pemba na mwandishi wa makala haya.