NA MARYAM HASSAN

WASTAAFU wa Wilaya ya Kati wameushukuru Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) kwa kuwasogozea huduma karibu na maeneo yao.

Wastaafu hao waliyasema hayo mara baada ya kumaliza zoezi la uhakiki ambapo (ZSSF) ilifika Dunga TC kwa lengo la kutekeleza wajibu wao.

Fatma Ramadhan, alisema apo awali walikuwa wanasumbuka kufuata huduma ya uhakiki kwa sababu ya uzee na wengine ni wagonjwa.

“Hii kwetu ni faraja kubwa sana kwa sababu huduma hii tulikuwa tunaifata Mjini, lakini leo tumesogezewa mpaka wilaya ya Kati kwa kweli ni jambo la faraja” alisema mama huyo.

Mbali na kusogezewa huduma wameiomba serikali kuwaongezea pencheni kwa sababu kipato wanachokipata hakikidhi mahitaji yao ya kila siku hasa ukizingatia tayari wameitumikia serikali kwa kipindi kirefu.

Jaalia Othman Mkali, mkaazi wa Kiboje, wameishauri ZSSF kutoa maelekezo sahihi kwa vituo ambavyo zitafanyika uhakiki, ili kuwaondolea usumbufu.

Vuai Juma Mwalim, alisema kusogezewa huduma hiyo kunawafanya kufika mapema, ili kuwahi kufanya kazi zao za kijamii.

Alisema kipindi cha nyuma walikuwa wakipata huduma hiyo Karikoo jambo ambalo huwafanya kushindwa kufanya kazi zao.

“Kipindi uhakiki unafanyika Mjini kulikuwa na msongamano mkubwa na baadhi yetu tupo wagonjwa lakini hivi sasa tunashkuru huduma hii kuipata katika wilaya yetu” alisema.

Aidha, alisema kitendo cha kutoa maamuzi kwa wazee wasiojiweza kubaki nyumbani na kuleta wawakilishi wao nalo limeweza kupunguza msongamano.

Raya Hamdani Khamis, Ofisa Mwandamizi Masoko na Uhusiano katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, alisema kwa Wilaya hiyo wanatarajia kuhakiki wastaafu zaidi ya 4,000.

“Hatutakua na idadi kamili katika Wilaya hii kwa sababu wazee wengi wamekuwa wakihama hama kwa hiyo hawa walioyopo ndio tunataraji kuwahakiki na kufikia idadi hiyo” alisema.