NA ASYA HASSAN

MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), inawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kutoa rushwa ya shilingi milioni 2.5 kwa Mtendaji wa juu wa Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi (ZFDA).

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi na Operesheni, Nasir Ahmed Haji, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mnazi Mmoja wilaya ya Mjini, Unguja.

Kaimu huyo alisema hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa ZAECA, alisema watu hao ni wafanyakazi wa kampuni ya IASIMJI ambao walitoa kiasi hicho cha fedha kwa Mkurugenzi wa juu wa taasisi hiyo kwa lengo la kuruhusiwa ama kubadilishiwa majibu ya vipimo vya mchele.

Kaimu huyo alifahamisha kwamba bidhaa hiyo ilikuwa makontena matano ya tani 130 ambayo yalishafanyiwa uchunguzi na taasisi hiyo na kuonekana haufai kwa matumizi ya binadamu.

Akiwataja watuhumiwa hao, kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IASIMJI Traders, Imrani Amini Simji (34) mkaazi wa Mbweni, Moise Saifdin Muhsin (28) mkaazi wa Darajani anaejishughulisha na shughuli za ‘Clearing and forwarding’ na mtuhumiwa wa tatu ni Raymond John Ribondo (31) mkaazi wa Kinondoni Dar es Salaam ambae ni dereva wa taxi.

“Watu hao baada ya kupatiwa majibu hayo waliamua kufanya hivyo ili uonekane mchele huo unafaa kutumiwa na binadamu,” alisema.

Aidha alifahamisha kwamba uchunguzi zaidi juu ya watu hao unaendelea na utapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo pamoja na kutoa taarifa pale wanapobaini kuna mwanya au harufu yoyote ya rushwa ili wahusika waweze kushughulikiwa.

Alifahamisha kwamba rushwa ni hatari na ina athari kubwa kwa jamii hivyo mashirikiano ya pamoja baina ya serikali na wananchi ndio yatakayoweza kuzaa matunda ya kutokomeza vitendo hivyo.