Waahidi uwajibikaji, utendaji uliotukuka

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha viongozi mbali mbali aliowateuwa hivi karibuni katika taasisi za serikali.

Walioapishwa ni Mussa Haji Ali kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Habiba Hassan Omar kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Issa Mahfoudh Haji kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.

Wengine ni Aboud Hassan Mwinyi kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango anaeshughulikia fedha na mipango wakati Mikidad Mbarouk Mzee aliapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.

Wakimzungumza mara baada ya kiapo hicho, viongozi hao waliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi ili kurudisha imani waliyopewa na Dk. Mwinyi kwa kuwateua kushika nyadhifa hizo na kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Dk. Habiba Hassan Omar alisema kazi aliyopewa inahitaji utendaji na uadilifu hivyo aliahidi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu uliopo ili kupeleka mbele maendeleo ya Zanzibar kulingana na matarajio walionayo wananchi kwa serikali yao.

“Wizara ninayoenda kuitumikia inakamata milango mikuu ya uchumi wa nchi yetu, hivyo lazima tukafanye kazi, kuimarisha uwekezaji, uchumi na vitu vyote muhimu katika uchumi wa taifa,” aliongeza Dk. Habiba.

Kwa upande wa sekta ya uchumi alisema atahakikisha wanashirikiana pamoja na watendaji wengine wa wizara yake kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, vikundi na taifa kwa ujumla.

Alisema atafanya hivyo kupitia sekta mbali mbali ikiwemo mikopo ya mabenki, miradi ya mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) na vyama vya ushirika kwa lengo la kusogeza mbele uchumi wa wananchi.