BERLIN, UJERUMANI

HALI ya hewa imeendelea kuwa mbaya nchini Ujerumani ambapo watu zaidi ya 30 wamekufa na wengine kadhaa hawajulikani walipo.Inaelezwa kuwa miongoni mwa waliokufa walikuwa wazima moto wawili.

Serikali ya nchi hiyo imepeleka wanajeshi kwenye sehemu zilizoathirika zaidi huku kukiwa na hofu huenda idadi ya vifo ikaongezeka wakati juhudi za kuwahamisha watu zinaendelea.

Watu waliokufa walishindwa kuondoka mapema kwenye sehemu zilizokumbwa na mafuriko za magharibi mwa Ujerumani.

Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku nzima.

Aidha baadhi ya nyumba zilizolewa na mafuriko huku ikielezwa kuwa, watu kati ya 50 mpaka 70 hawajulikani waliko.

Idara kuu ya utabiri wa hali ya hewa imetahadhrisha juu ya mvua kubwa kuendelea kunyesha itakayoandamana na dhoruba na kwamba mvua hizo zitaendelea.

Kansela Angeka Merkel aliyeko safarini amesema amewasiliana na wizara za mambo ya ndani na fedha kutoa misaada pale itakapohitajika.