NA MARYAM HASSAN

IKIWA zimepita siku chache Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, kushiriki zoezi la kuangamiza dawa za kulevya nchini huko Mahonda, kitengo cha kupambana na dawa hizo kimemmkata kijana wa miaka 55 akiwa na vijiwe tisa vyenye uzito wa gramu 0.930.

Mkuu wa Kitengo hicho, Omar Khamis, ambae pia ni mrakibu wa Polisi, alisema kijana Yussuf Mohammed Yussuf, mkaazi wa Saateni alikamatwa kufuatia msako uliofanywa na askari wa kitengo hicho.

Aidha alifahamisha kuwa mtuhumiwa akiwa na kifuko cha plastiki ndani yake mkiwa na unga mfumo wa vijiwe akiwa amekihifadhi kwenye huksi ya suruali.

Alisema bado mapambano yanaendelea ya kuwasaka waingizaji wasambaji na watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuhakikisha wanawafikisha katika vyombo vya sheria.

Alifahamisha kuwa mnamo Julai 5, mwaka huu majira ya saa 5:30 asubuhi huko Kwarara kwa Ngurangwa walifanikiwa kumkamata Hamid Said Saudi (32) mkaazi wa Kidongo Chekundu mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema kijana huyo alikamatwa na furushi la gazeti ndani yake mukiwa na nyongo 250 za majani makavu zilizotiliwa mashaka kuwa ni bangi.

Aidha alisema askari wa kitengo H.7804 D /C Idirissa alimkamata Jabir Ali Said (29) mkaazi wa Kilimahewa mkoa wa Mjini Unguja, akiwa  na kikoba rangi nyekundu ndani yake mukiwa na nyongo 250 za majani makavu zilizotiliwa mashaka kuwa ni bangi.