NA MWANAJUMA MMANGA
MWAKILISHI wa Jimbo la Fuoni, Yussuf Hassan Iddi, amesema juhudi zaidi zinahitajika za kuwahamasisha wazee umuhimu wa kupima afya mara kwa mara, ili kuwakinga na maradhi yanayoweza kuepukika
Iddi, aliyasema hayo wakati akizindua mabaraza ya Wazee wa Shehia ya Fuoni Kipungani na Migombani, ulioambatana na upimaji wa afya kwa wazee na kukosekana kwa huduma za afya ikiwemo vipimo kwa wazee kunasababisha kupata maradhi sugu hivyo ni vyema jamii kuwa karibu nao kwa uangalizi zaidi wa kiafya.
Alisema hatua hiyo ya upimaji wa afya kutasadia kutambua maradhi yanayokusumbua iwapo mtu atachunguza mara kwa mara, kwani wazee wanawakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukumbwa na maradhi ya shindikizo la damu, sukari, macho, miguu pamoja na kutengwa na jamii ukifikia umri wa uzee.
‘Niwaombe sana kinamama kupokea matibabu hayo na dawa, ili kuendelea kupata afueni na inshaalla afya zitarudi katika hali yake ya kawaida” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ameamua kuekwa chombo cha baraza la wazee, ili kuwa na sauti moja ambayo wataweza kusemea na kutatulia changamoto zao ziweze kufanyiwa kazi na amezitaka taasisi zinazota msaada wa huduma za afya kujitokeza, ili kuwasaidia wazee wa eneo hilo.
Nae Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Magharib ‘B’, Khamis Hassan Juma, alisema lengo la upimaji afya huo ni kuhakikisha wazee wanapata mwamko wa kujua afya zao na kuweza kupatiwa matibabu sahihi na kwa wakati endapo atakuwa na tatizo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa maradhi ya kisukari na masuala ya lishe Salama Asaa Ali, alisema miongoni mwa maradhi waliyogundua yanawasumbua wazee wengi ni shindikizo la damu na kisukari na aliwataka wazee kupuepuka kutumia vyakula vinavyosababisha kupata maradhi hayo.
Nao wazee waliopimwa afya zao na kupatiwa matibabu wameuomba uongozi wa jimbo la Fuoni kuendeleza kambi za madaktari, ili kupata urahisi wa kupima afya zao na wamemshukuru Mwakilishi kwa kuwasaidia kupata matibabu hayo na kumtaka kuenelea kuwasaidia matibabu ya maradhi mengine.