NA ABOUD MAHMOUD

MAJAJI na mahakimu nchini wametakiwa kuwa makini na kutenda uadilifu katika kazi zao ili kuondosha lawama kati yao na wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, wakati alipofanya ziara na kukutana na watendaji hao katika jengo la Mahakama kuu lililopo Vuga.

Waziri Haroun alisema endapo kutakuwepo kwa umakini na uwajibikaji wa masuala ya kesi za udhalilishaji na dawa za kulevya kutapunguza mambo hayo ambayo yanasababisha kilio kikubwa kwa wananchi.

“Wito wangu kwenu majaji na mahakimu kufanya kazi zenu mkiwa na umakini mkubwa na kutenda uadilifu ili kuepukana na lawama zinazotoka kwa wananchi, naamini kufanya hivyo hata kesi za udhalilishaji na ubakaji zitapungua,” alisema.

Sambamba na hayo waziri Haroun alisisitiza kuendelea kupiga vita suala la udhalilishaji na dawa za kulevya kwa kuchukuliwa hatua madhubuti za kisheria ambazo zitasaidia kuondosha matatizo yanayoikabili jamii kwa ujumla.

Naye  Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alisema kutokana na uhaba wa nafasi katika jengo la mahakama kuu ndio inayosababisha kuwepo kwa  uzorotaji wa kuendesha kesi mahakamani.

Alifahamisha kwamba kukiwepo na jengo kubwa ambalo litakua na sehemu ya kutosha ya kufanyia kazi tatizo hilo halitokuwepo wala kujirudia tena.

“Tatizo linalotukabili linatokana na uhaba wa nafasi katika jengo hili la mahakama hii inachangia kuwepo kwa uzoroteshaji wa kuendesha kesi Imani yangu tukipata jengo lenye nafasi tatizo hilo halitojitokeza tena,”alisema Makungu.

Naye Mrajis wa Mahkama Mohamed Ali Mohamed alisema juhudi mbali mbali zinachukuliwa kuhakikisha masuala ya udhalilishaji yanapungua na tatizo la uchukuaji ushahidi na utoaji maelezo unafanyiwa kazi ili kuhakikisha kesi zinatolewa ufumbuzi kwa haraka.

Kwa upande wake Naibu Mrajis, Yessaya Kayange alisema suala la mashahidi kufika mahamani ni tatizo ambalo huzorotesha kesi za udhalilishaji kwenda kwa haraka.

Alifahamisha kwamba wapo tayari kufuata sheria na kushirikiana na Serikali, katika kutatua changamoto mbali mbali za kimahakama.