NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema kuwa kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), kuwa ndio shirika pekee lenye mamlaka ya kununua karafuu za Zanzibar moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi ya karafuu kwa mwaka 2021/2022, iliyofanyika bandarini Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa hakuna taasisi au chombo chengine kilichopewa mamlaka ya kununua karafuu za Zanzibar moja kwa moja kutoka kwa wakulima zaidi ya shirika la ZSTC.

Hivyo alipiga marufuku tabia ya wananchi kuuza karafuu kwa mtu mwengine yoyote, hivyo wanapaswa kutambua kuwa ZSTC haina madalali wala mawakala iliowatuma kununua karafuu hizo.

“Serikali imeweka utaratibu mzuri karafuu kuziuza kwa wakati tena salama, ZSTC ndio sehemu pekee ya kuuzia karafuu hizo tena wanazifuata popote zilipo”, alisema.

Akizungumzia suala la dhamana kwa wanaopasisha na kuweka ubora, aliwataka kutambua wamepewa dhamana kubwa hiyo, kuhakikisha wanatekeleza dhamana zao bila ya kumuonea mkulima wala kujionea wao katika upasishaji na upandishaji wa gredi.

Alisema bado karafuu ya Zanzibar inaendelea kuwa muhimu katika soko la dunia, hivyo aliwataka wakulima kuhakikisha wanachuma zikiwa zimepea, pamoja na kuzianika katika mazingira mazuri ili kulinda ubora wake.

“Kumejitokeza tabia ya watu kuzichuma karafuu changa, hilo lisifanywe maana halimsaidii mmiliki, bali tunapaswa kuwa na uzalendo kwa nchi, kama karafuu hazijawa tayari tunapaswa kuziacha mpaka zipee ili tusipoteze hadhi ya karafuu yetu kwani kila nchi inajivunia vitu vyake”,alisema.