PORT-AU-PRINCE, HAITI

WAZIRI Mkuu mpya wa Haiti, Ariel Henry ameahidi kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo kufuatia kuuwawa kwa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jovenel Moise.

Katika kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari, Henry alisema mpango wa serikali yake ni kufanikisha uchaguzi huru, wa kuaminika, wenye uwazi na ambao utawashirikisha wapiga kura wengi huku akisisitiza kuhusu haja ya usalama nchini humo.

Pia alizungumzia takwa la kukabiliana na tatizo la ajira na kuujengea uwezo mfumo wa kimahakama na kuongeza kuwa amekutana na viongozi wa asasi za kiraia tangu alipokula kiapo chake Julai 20.

Mkutano huo ambao ulidumu kwa takribani dakika kumi, ulifanyika katika kipindi cha tofauti ya masaa machache baada ya Henry kukutana na baraza lake jipya la mawaziri katika mkutano wa ndani.

Katika mkutano huo, inatajwa kwamba alitoa taarifa ya maendeleo ya uchunguzi wa mauaji ya Julai, 7 ya Rais Moise.

Kiongozi huyo aliuwawa akiwa katika makaazi yake binafsi ambapo pia mke wake alijeruhiwa vibaya.