NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Raisi, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mpango madhubuti katika sekta ya uwekezaji ili kuona sekta hiyo inakuwa na kuleta ufanisi uliokusudiwa.

Akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Mashiriki wa Taasisi ya Elsewedy Eletric, Ibrahim Qamar na Credo Amouzouvik kutoka Credo Group iliyopo nchini Marekani wanaoshughulika umeme wa jua, walipofika Ofisini kwake Mwanakwerekwe Mjini Unguja kwa kujitambulisha.

Waziri Soraga, alisema Zanzibar imeweka mazingira mazuri katika sekta hiyo na ina maeneo mengi ya kuwekeza yakiwemo ya Uchumi wa Bluu wa Utalii.

Aidha, alisema hivi sasa kumekuwa na vituo maalum One Stop Center, ambacho kimekusanya taasisi zote zinazoshughulikia uwekezaji ambapo ndani ya siku muekezaji anakamilisha taratibu zote zikiwemo upatikanaji wa kibali.

Alifahamisha kwa upande wa wawekezaji wanaotaka kuwekeza Zanzibar wanakaribishwa katika maeneo mbali mbali ya vitega uchumi ambayo yatawavutia kwa kuekeza.

Nae,  Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Mashiriki wa Taasisi ya Elsewedy Eletric, Ibrahim Qamar, alisema alivutiwa na ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.