TOKYO, JAPAN

WAZIRI wa Mambo ya nje wa Japani, Motegi Toshimitsu anapanga kuitembelea Iran katikati ya mwezi Agosti mwaka huu ikiwa ni mapema zaidi ili kukutana na maofisa waandamizi wa serikali mpya ya nchi hiyo iliyopo ghuba ya uajemi.

Motegi huenda akazuru nchi hiyo baada ya kiongozi mwenye msimamo mkali asiyependa mabadiliko na anayeipinga Marekani, Ebrahim Raisi kuchukua mamlaka kutoka kwa rais wa sasa, Hassan Rouhani, mapema mwezi Agosti.

Msomi huyo wa kiislamu na mkuu wa zamani wa mahakama alishinda uchaguzi wa urais nchini Iran mwezi uliopita.

Katika mikutano na waziri mpya wa mambo ya nje wa Iran na viongozi wengine wa serikali ya Raisi, Motegi anatarajiwa kuwasihi kutekeleza jukumu muhimu katika jitihada za kupunguza hali ya wasiwasi na kuleta uthabiti katika eneo la mashariki ya kati.

Motegi na maofisa wa Iran huenda wakajadili mazungumzo yasiyokuwa ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuhusiana na makubaliano ya mpango wa nyuklia ya mwaka 2015.

Hivi sasa shutma zimeanza kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya dhidi ya Iran kuanza tena urutubishaji wa madini ya uranium kwa asilimia 20 kinyume na makubaliano ya kimataifa yaliyokubaliwa mwaka 2015, hivyo ziara ya waziri hiyo inaumuhimu wa kipekee.

Kadhalika katika ziara yake hiyo Motegi anapanga kuzitembelea nchi kadhaa katika eneo la mashariki ya kati zikiwemo Israel, Palestina, Misri, Jordan, Uturuki, Iraq na Qatar.