TUNIS, TUNISIA
RAIS Kais Saied wa Tunisia amemfukuza kazi waziri wa ulinzi, ikiwa siku moja baada ya kumuonda waziri mkuu na kulisimamisha bunge, na hivyo kuiingiza demokrasia changa ya taifa lake katika mgogoro wa kikatiba.
Rais huyo alitangaza kuwaweka pembeni Waziri wa Ulinzi Ibrahim Bartaji na Hasna Ben Slimane ambae alikuwa akikaimu nafasi ya waziri wa sheria.
Hayo yanatokea baada ya kuzuka machafuko nje ya eneo la bunge lilikuwa likidhibitiwa na jeshi, baada ya Saied kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kuamuru bunge kufungwa kwa siku 30, hatua ambayo chama kikubwa cha kisiasa nchini humo cha Ennahada imeiita kama kitendo cha mapinduzi.
Uamuzi uliowashangaza wengi wa Rais Saied unafanyika katika kipindi cha takribani muongo mmoja tangu mapinduzi ya Tunisia ya 2011, ambayo yalikuwa chachu ya vuguvugu la mataifa ya Kiarabu.