KIGALI, RWANDA

WAZIRI wa zamani wa Rwanda Augustin Ngirabatware, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda, sasa atatumikia kifungo chake kilichobaki nchini Senegal.

Hayo yameelezwa na mawakili wake aliopo mjini The Hague.

Inaelezwa kuwa mnamo Mei 28, Jaji Carmel Agius wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, MICT alisema amemuelekeza msajili wa mahakama amuhamishie Ngirabatware nchini Senegal ili kutumikia adhabu yake.

Ngirabatware aliyewahi kuwa waziri wa mipango wakati mauaji ya kimbari yanafanyika, ambapo Watusti 800,000 na Wahutu wachache waliuawa kati ya Aprili na Julai mwaka 1994.

Alihukumiwa Desemba mwaka 2012 kwa kuchochea, kusaidia na kuwahamasisha wapiganaji wa Kihutu katika wilaya ya Nyamyumba kaskazini magharibi mwa Rwanda kuwaua na kuwabaka majirani zao wa Kitutsi.

Hukumu ya awali ya miaka 35 jela ilipunguzwa hadi 30 mnamo mwaka 2014, baada ya kuondoshewa kesi ya ubakaji.