KWA mara nyengine tena mahujaji wa Zanzibar na sehemu nyengine duniani walioweka nia wameshindwa kwenda kutekeleza ibada ya hijja ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu sana za dini ya kiislamu.
Ili ukatekeleze ibada ya hijja kwanza lazima uweke nia, lakini jambo jengine muhimu uwe na uwezo wa kifedha wa kufika kwenye maeneo yanayotekelezwa ibada hiyo.
Hijja ni nguzo ya tano katika dini ya kiislamu, ambapo ibada hiyo ni tofauti na faradhi nyengine za dini hiyo, kwa sababu hutekelezwa nchini Saudi Arabia kwenye miji na maeneo maalum.
Sababu kubwa ya mahujaji wa Zanzibar na sehemu nyengine ulimwenguni kwa mwaka huu kushindwa kwenda kutekeleza ibada hiyo ni janga la ugonjwa wa corona linalosumbua maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Corona limekuwa tatizo la kiulimwengu kwani ni ugonjwa unaosambaa kwa haraka sana na bila ya kuwepo kwa karantini kwenye nchi mbalimbali ugonjwa huo unaweza kuathiri maisha ya watu wengi.
Kama ilivyokuwa kwa mwaka uliopita, mwaka huu pia ibada hiyo inafanywa na waumini wachache walioko ndani ya Saudi Arabia kwa hofu ya kusambaa maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Pamoja na wanasayansi ya afya kugundua chanjo huku mamilioni ya watu wakiwa wameshapatia chanjo za ugonjwa huo, bado mtihani wa ugonjwa wa corona umeendelea kuwepo kwani katika baadhi ya nchi zimeshapigwa na mawimbi matatu, huku maelfu ya watu wakifariki dunia.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijiandaa kuwapitia mahujaji chanjo ya corona, lakini kama nchi ya Saudi Arabia ingeruhusu mahujaji kuingia nchini humo kwa sharti kwamba wamepimwa hawana maambukizi na wamepatiwa chanjo.
Lakini baadae taifa hilo liliopo mashariki ya kati lilitoa muongozo mpya wa kuzuia kabisa mahujaji kuingia nchini humo na kwamba ibada ya hijja itatekelezwa na watu wachache waliomo nchini humo.
Lakini kwa Zanzibar wapo waumini waliokwisha jiandaa kihali na kimali pengine kwa zaidi ya mzima kwenda utekeleza ibada hiyo, hivyo ushauri wetu ni kwamba wazidishe maandalizi maradufu kwa ajili ya mwakani.