Kuanza kutolewa rasmi kesho kutwa
NA MADINA ISSA
WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imekabidhiwa chanjo na vifaa vitakavyotumika kwenye zoezi la utoaji wa chanjo kipindupindu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).
Zoezi hilo la chanjo litaendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza linatarajiwa kufanyika Julai 3 mwaka huu ikiwahusisha wananchi zaidi ya 327,000 wanaosihi katika shehia hatarishi za uwepo wa ugonjwa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alisema serikali kupitia wizara yake inalishukuru Shirika hilo kwa msaada wa chanjo hiyo pamoja na vifaa.
Aidha Mazrui alisema wizara yake na serikali ya Mapinduzi kwa ujumla itaendelea kushirikiana na shirika hilo katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi.
Alisema katika mkakati wa serikali ya kuondosha ugonjwa wa kipindupindu Zanzibar, WHO imeona ipo haja ya kuisaidia Zanzibar kwa kuipatia misaada mbalimbali ikiwa na lengo la kuhakikisha ugonjwa huo unakuwa historia.
“Shirika la WHO limekuwa na jitihada mbalimbali katika kuisaidia Zanzibar katika kuhakikisha matatizo mbalimbali ya kiafya kwa wananchi yanaondoka”, alisema.
Aidha alisema, kupatiwa chanjo hiyo kutasaidia Zanzibar kupungua kwa maradhi ya mripuko ya kipindupindu katika shehia zinazosifika kwa ugonjwa huo ambapo alisema kukabidhiwa vifaa hiyo kutasaidia kutangaza vyema jinsi ya kujikinga na miripuko.
Hivyo, aliliomba shirika hilo, kuendelea kuisadia Zanzibar kwani wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ambapo wananchi wamekuwa wakifaidia na shirika hilo.
Sambamba na hayo, aliwataka wananchi kwenye shehia zitakazohusika na zoezi hilo kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha malengo ya serikali kutokomeza kipindupindu hapa Zanzibar.
Nae Mwakilisha mkaazi wa Shirika la Afya duniani Ofisi ya Zanzibar, (WHO), Dk. Andemichael Ghirmy, alisema shirika hilo litaendelea kutoa msaada mbalimbali kwa wananchi wa Zanzibar.