TOKYO, Japan

Tedros Adhanom Ghebreyesus,

MKUU wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema, michezo ya Olimpiki ya Tokyo inapaswa kuendelea ili kuudhihirishia ulimwengu kile kinachowezekana kwa kuzingatia mipango na hatua sahihi.

Katika hotuba yake kwenye kikao cha wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki mjini Tokyo, Tedros, amesema, ulimwengu unahitaji kwa sasa michezo ya Olimpiki kama ‘sherehe za matumaini’.

“Mbali na mashindano, medali na rekodi, michezo hiyo inayaleta mataifa ya ulimwengu pamoja katika kusherehekea, urafiki na heshima, lakini, mwishowe ni sherehe ya kitu muhimu zaidi ambacho dunia inahitaji sasa kuliko wakati mwengine”, alisema, Tedros
Michezo ya Tokyo inaanza leo Ijumaa Julai 23 wakati kukiwa na maswali kuhusu usalama wake huku maelfu ya wageni wakiwasili.

Tedros amekosoa kuwepo kwa utofauti kati ya nchi, akisema, janga hilo lingemalizwa kama mataifa tajiri ya G20 yangeonyesha uongozi wa pamoja na kuwepo na usambazaji wa haki zaidi wa chanjo.

“Janga la ‘corona’ limetuuliza maswali mengi kutuhusu na kuhusu ulimwengu wetu. Janga hili ni mtihani na ulimwengu unafeli.
“Zaidi ya watu milioni nne wamekufa na zaidi wanaendelea kufa. Tayari mwaka huu idadi ya vifo ni zaidi ya maradufu ya idadi ya jumla ya mwaka jana”, aliongeza, Mkuu huyo wa WHO.

Michezo ya Olimpiki ambayo iliahirishwa mwaka jana kutokana na ‘corona’, itafanyika bila ya mashabiki viwanjani ili kupunguza kitisho cha afya.

Mpaka sasa kumekuwa na zaidi ya visa 67 vya maambukizi ya ‘corona’ COVID-19 nchini Japan miongoni mwa waliopewa vibali vya kushiriki mashindano hayo tangu Julai 1, licha ya kuwepo hatua kali za kuingia nchini humo.

Kufikia juzi, kulikuwa na visa 1,287 vya maambukizi mjini Tokyo. Hata hivyo,Tedros, amesema michezo hiyo haipaswi kuhukumiwa na idadi ya visa vya ‘corona’ vinavyojitokeza kwa sababu haiwezekani kamwe kuondoa kitisho.

Alisema jinsi maambukizi yatakavyoshughulikiwa ndicho kitu cha msingi.
Rais wa Kamatifa ya Kimataifa Olimpiki (IOC), Thomas Bach ameapa kuendelea kupambana na janga la ‘corona’ kupitia michezo, licha ya ukosoaji kuwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo inafanyika wakati kukiwa na ongezeko la maambukizi nchini Japan
Idadi ya visa vinavyohusishwa na tamasha hilo nchini Japan mwezi huu ilifikia 79 juzi huku wanamichezo zaidi wa kimataifa wakigunduliwa kuwa na maambukizi katika nchi zao na kushindwa kusafiri.