NAIROBI, KENYA
USAMBAZAJI wa chanjo ya virusi vya Corona barani Afrika umeongezeka kwa kasi, na kuweka chachu mpya katika juhudi za bara hilo kudhibiti maambukizi na idadi ya vifo vinavyotokana na virusi hivyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti alisema, karibu dozi milioni nne za chanjo hiyo ziliwasili barani Afrika wiki iliyopita, wakati mipango ya kuongeza kasi ya upatikanaji na utoaji wa chanjo kwa asilimia 30 ya idadi ya watu barani humo ikishika kasi.
Mkurugenzi huyo alisema, dozi milioni 79 za chanjo ya virusi vya Corona tayari ziliwasili barani Afrika, na watu milioni 21 ambao ni sawa na asilimia 1.6 ya watu barani humo wamepata chanjo kamili.
Alisema kuwa, Afrika inahitaji dozi milioni 820 za chanjo ya virusi vya Corona ili kuchanja asilimia 30 ya watu barani humo itakapofikia mwisho wa mwaka huu.