Jamii haipaswi kupuuza, Ni baya zaidi kuliko yaliyopita
Serikali zote mbili zatoa tahadhari
NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)
UGONJWA wa corona ulioibuka mwishoni mwa mwaka 2019 nchini China, bado unaisumbua dunia licha ya kuwepo chanjo mbalimbali kwa kuwa bado wapo watu wanaougua na wanaofariki kwa ugonjwa huo.
Hivi sasa linatajwa ni wimbi la tatu la corona jambo ambalo kila nchi lina utaratibu na miongozo yake jinsi ya kukabilina na ugonjwa huo.
Kwa mfano hivi karibuni Serikali ya Tanzania imesema kuna viashiria vya wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19 kutokana na virusi vya ugonjwa huo kuingia nchini humo kutokea nchi jirani.
TAHADHARI DHIDI YA CORONA ILIYOLEWA NA SMT
Mkurugenzi wa kinga wa Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi alitoa maagizo kadhaa likiwemo la kuwataka wananchi kuvaa barakoa. Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa mwezi uliopita.
“Wizara inawakumbusha wananchi wote kutopuuza ugonjwa wa Covid-19. Wizara imeanza kuona viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la mlipuko wa ugonjwa huu katika nchi yetu.” Mkurugenzi huyo amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akiyasema hayo.
“Hii ni kutokana na taarifa za ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa huu zinazofanywa na wizara na mwingiliano kati ya watu wetu na mataifa mengine,” amesema Dk Subi.
Aliongeza kwamba idadi ya wagonjwa wanaopatikana na vizuri vya corona barani Afrika imeongezeka ndani ya wiki tano mfululizo zikiwemo nchi zinazopakana na Tanzania, “maambukizi yanaongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa wimbi la pili.” Alitoa nukuu hiyo.
Katika maelezo yake aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kutumia sabuni.
Daktari Subi hatahivyo hakutoa takwimu za idadi ya raia wa Tanzania ambao wamepatikana na ugonjwa huo hadi kufikia sasa na haijajulikana Iwapo mamlaka zitatekeleza maagizo ya kuwazuia watu kukaribiana au kukusanyika .
Ilani hiyo ya serikali imejri wakati ambapo mataifa jirani ya Kenya na Uganda yamechukua hatua Zaidi kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Kwa upande wake Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeungana na nchi nyengine za Afrika kuchukuwa tahadhari dhidi ya wimbi la tatu ugonjwa wa Corona unaozidi kuitesa dunia kwa takriban mwaka sasa.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alitoa taarifa kupitia mkutano na waandishi wa habari kuwa tayari kuna dalili za kuongezeka kwa corona na kuwataka kuchukuwa tahadhari kwa kuvaa barakoa na kuepusha mikusanyiko isiyo na lazima.
Mbali na hilo alisema tahadhari nyengine ni kuwapima watu wanaoingia na kutoka nchini huku wananchi wakitakiwa kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima katika kipindi hiki ambacho ni hatari kwa afya zao.
Alisema awamu ya tatu ya wimbi la Corona Zanzibar bado ipo salama hadi sasa kwa sababu hakuna mgonjwa hata mmoja aliejitokeza kupitia vituo vya uchunguzi kwa watu wanaoingia na kutoka Zanzibar, wakiwemo watalii kutoka mataifa mbalimbali ya ulaya na Afrika lakini hata hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari.
“Napenda kuwajuilisha wananchi kwamba Wizara imepata taarifa kutoka vyanzo mbali mbali juu ya kuwepo viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya Korona nchini”, alisema Mazrui.
Alisema hilo limetokana na kuongezeka sana kwa maambukizi kwa baadhi ya nchi zikiwemo Uganda, Afrika Kusini na Jamhuri ya watu wa Congo ambazo watu wan chi hizo wamekua na muingiliano mkubwa kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Kutokana na hali hiyo, Wizara haina budi kuimarisha zaidi mikakati ya kinga na kujiweka tayari dhidi ya hali hiyo mara tu itakapotokea, kufuatia kuendelea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Korona na kwa kuzingatia wimbi la tatu la ugonjwa huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto inatoa taarifa ya tahadhari ya kuwepo kwa ugonjwa huu unaosambaa kwa kasi kubwa. Wizara imo katika taratibu za kuweka miundo mbinu na rasilimali watu katika kila hospitali kwa lengo la kujiandaa iwapo mripuko wa ugonjwa huu utajitokeza” alieleza Waziri Mazrui.
MIKAKATI YA SMZ YA KINGA DHIDI YA CORONA
Hata hivyo alisema kuwa wizara imejianda na kujitayarisha na kinga dhidi ya ugonjwa huo kwa Kuimarisha kinga na udhibiti wa uingiaji wa maradhi katika mipaka (point of entry), kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakuja na vyeti vya uthibitisho wa kutokua na maambukizi na kuwa wageni wote wanaoingia nchini ambao wanatoka katika nchi hatarishi zaidi wanafanyiwa kipimo cha haraka.
Akizitaja nchi hizo Waziri Mazrui alisema nchi husika kwa sasa ni India, Afrika Kusini, Uganda, DR Congo, Uingereza, Marekani, Peru, Phillipines na Brazil zote hizo ndizo zilizogundulikana kuwa na aina mpya ya virusi vya Korona.
Kuimarisha ufuatiliaji na ugunduzi wa awali wa wagonjwa katika mipaka ikiwemo kuwapima joto la mwili kwa kutumia “walk through thermoscan” ni sehemu ya kujikinga na maradhi ya Corona hivyo kila jitihada zinafanyika ili kuweka Zanzibar na watu wake kuwa salama.
UTOAJI WA ELIMU DHIDI YA CORONA ZANZIBAR

Akizungumzia namna ya utoaji wa elimu ya afya kwa Jamii Waziri Mazrui alisema Kitengo cha Elimu ya Afya ya jamii kitatoa matangazo mbali mbali kupitia redio na Televisheni za serikali na binafsi na utaratibu wa kutumia mitandao ya kijamii pia itatumika, matangazo ya mitaani (Bill boards/Banners) elimu katika skuli pia yatapewa kipaumbele ili jamii ielimike katika suala hilo.
Aidha Waziri huyo alisema wizara itaongeza usimamizi juu ya ufuataji wa miongozo ya kinga iliyopo katika ngazi mbali mbali ikiwemo kukaa umbali usiopungua mita moja baina ya mtu na mtu, matumizi ya maji salama kwa kukosha mikono au kutumia vitakasa mikono, matumizi ya Barakoa, kuepuka kupeana mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwa kipindi hiki cha tishio la ugonjwa huo.
Akizitaja hatua nyengine zitakazochukuliwa dhidi ya ugonjwa huo ni kuweka utaratibu maalumu katika vituo vya afya na hospitali juu ya ugunduzi wa mapema kwa washukiwa wa maradhi haya “triage system”, kuongeza ufuatiliaji na uchunguzi kwa makundi hatarishi zaidi wakiwemo wagonjwa wenye maradhi sugu kama vile Kisukari, maradhi ya moyo na Wazee wenye umri mkubwa.
Aidha waziri Mazrui alisema kunafanywa matayarisho katika ngazi ya Hospitali zote za Unguja na Pemba, kuhakikisha uwepo wa sehemu maalumu za kuwahifadhi na kuwatibu watu watakaosadikiwa kua na ugonjwa katika kila hospitali za Serikali na Binafsi.
Sambamba na hilo, lakini alisema kupima watu wote wenye dalili za ugonjwa wa corona kwa kutumia kipimo cha haraka , kuimarisha vikosi kazi vilivyopo katika kila Wilaya na hospitali juu ya kujiweka tayari na wimbi la tatu la maambukizi na kuimarisha mawasiliano na usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za kulazwa kwa kutumia nambari 196 na 0772 502 513.
Akijibu msimamo wa Zanzibar na chanjo ya Corona, Mazrui, alisema suala hilo ni la kitaifa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda kamati ya kitaalamu ya kufuatilia suala ya chanjo kabla ya kutoa maamuzi kuhusu kutumika kwa chanjo hiyo baada ya kuthibitika ubora na usalama wake.
“Chanjo itakapoanza kutumika baada ya kamati kumaliza kazi yake mimi nitakua wa kwanza kuchanjwa ili kuondosha khofu kwa wengine na kama ina madhara nianze kudhurika mimi lakini suala la chanjo litafanyika kwa uwazi na wananchi wataarifiwa rasmi bila ya kificho chochote” alisema Mazrui.
Alisema Serikali ipo tayari kupokea chanjo ya aina yoyote ya Corona lakini itakua tayari kutumia chanjo mpaka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano itakapotoa msimamo wa pamoja baada ya kamati ya wataalamu kumaliza kazi yake na kuwasilisha ripoti yao kwa Rais Samia.
Hata hivyo tangu Tanzania kusitisha kupima mwezi mei mwaka Jana hakuna wagonjwa waliolazwa hospitali wala hakuna takwimu zozote za wagonjwa wa corona.
NINI VIRUSI VYA CORONA
Virusi vya Corona ni mripuko mpya wa ugonjwa wa kuambukiza kwa njia ya hewa uliogunduliwa mwaka 2019 na havikuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa bindamu. Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi, shida katika kupumua, na katika hali ngumu zaidi, maambukizi yanaweza kusababisha, kukosa pumzi, kushindwa kufanyakazi kwa figo na hata kufariki dunia.
Virusi vya corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyojulikana kusababisha magonjwa yanayoanzia homa ya kawaida hadi homa kali kama vile Homa Kali ya Upumuaji ya Mashariki ya Kati (MERS) na Homa Kali ya Mfumo wa Upumuaji (SARS).
ISHARA NA DALILI ZA COVID19
Ishara na dalili Dalili hizi kawaida ni laini na huanza kwa hatua. Maumivu ya kichwa Vidonda vya koo Maumivu ya mwili Kutapika Kuhara Kikohozi kavu Homa Kupumua au kuhema kwa shida
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, ugonjwa huu wa wimbi la tatu unaweza kuua zaidi kuliko ule wa mawimbi mawili yaliyopita.
MAKUNDI HATARISHI YA KUUGUA CORONA
Makundi yaliyohatarini zaidi ni pamoja na wazee na wale walio na shida maalum za kiafya kama shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kisukari, maradhi ya kupumua kama pumu ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kukuza ugonjwa zaidi.
WANAVYOZUNGUMZA WATAALAMU WA AFYA
Akizungumza na makala haya Daktar bingwa wa magonjwa ya maskio, pua na mdomo kutoka hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ambae ni naibu mratibu wa matibabu na ufuatiliaji janga hili la corona kwa hapa Zanzibar, Massoud Hakim Bakari, alisema kuwa wananchi hawapaswi kupuuza ugonjwa huo.
“Baadhi ya wananchi wanapuuza kuchukuwa tahadhari juu ya wimbi la tatu la corona wakiendelea na mikusanyiko mikubwa ya watu kama vile misikitini, makanisani, maharusini, masokoni, mazikoni na hata maskulini na kwengineko huku wakiona kama ugonjwa haupo”, alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo inaonesha bado elimu inahitajika kuwakumbusha wananchi huku akitilia mkazo sehemu za mikusanyiko kama kwenye magari ya abiria, masokoni, kwenye vijiwe na viwanja vya michezo ni kama vile hawana taarifa kama kuna ugonjwa huo alisema.
Nae Daktar Huba Khamis Rashid Kutoka Skuli Ya Afya Sayansi Tiba, Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) alisema hili wimbi la tatu haliangalii umri wala ishara na daliliukilinganisha na wimbi la kwanza na lapili.
Daktar Huba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluh Hassan kwa kutamka rasmi kwamba kuna tatizo corona nchini na kwamba alitaka tahadhari ichukuliwe.
“Kwa kuwa viongozi wetu wanataka tahadhari zichukuliwe basi nasi hatunabudi kufanya hivyo kwani tatizo lipo kinyume na tunavyofikiria”, alisema.
Joe David Kanumbai Daktar na Muhadhiri kutoka SUZA alisema watu wenye homa, kikohozi na shida ya kupumua wasipuze kabisa hali hiyo wanapaswa kutafuta matibabu ya haraka.
Alisema ni vyema wakaenda hospitali kuangalia afya zao jambo ambalo linaweza kupata tiba ya mapema.
Daktar Joe aliwataka watu kuacha dhana potofu na kwamba virusi vya covid 19 haviwezi kusambazwa katika maeneo yenye hali ya hewa ya joto na yenye unyevu.
Kutokana na ushuhuda hadi sasa, virusi vya Corona vinaweza kusambazwa katika hali zote, pamoja na maeneo mengine.
“Hakuna ushahidi wa kisayansi ya madai haya kwamba kunywa maji moto ya malimau na kuweka unyevu wa mdomoni kutazuia kuambukizwa virusi vya corona. Lakini kunywa maji kunaweza kusaidia kuipa kinga yako nguvu kwani virusi huwashambulia kwa urahisi wale walio na mfumo dhaifu wa kinga”, alisema.