NA KHAMISUU ABDALLAH
WIZARA ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar imewataka wananchi wa Unguja na Pemba waliopewa hati ya umiliki wa ardhi kwa muda kuzirejesha hati hizo mara moja.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Maisara mjini Unguja.
Alisema lengo la wananchi kurejesha hati hizo ni kufuata sheria kwa kuomba tena ili waweze kupewa hati ya kukodishwa ardhi na kuona nao wawajibike kulipa kodi ya ardhi serikalini.
Aidha alisema wapo watu ambao walipewa hati za umiliki wa muda kwa ajili ya makaazi lakini eneo hilo wakalitumia kwa ajili ya biashara hivyo wanatakiwa waombe na kupewa hati ya kukodishwa ardhi kwa mujibu wa sheria.
“Kila mtu mwenye hati ya muda anatakiwa airejeshe na kuomba apewe hati ya kukodishwa ardhi ili nao wawajibike kulipa kodi ya ardhi serikalini na serikali iweze kupata mapato yake,” alibainisha.
Alifahamisha kuwa kipindi kirefu sasa kuna maeneo mengi ya Zanzibar serikali imekuwa ikikosa mapato yanayotakana na ukodishwaji wa ardhi ambayo yanatagemewa katika maendeleo ya nchi.
Katibu Kilangi alisema kwa kipindi kirefu serikali imekuwa ikikosa mapato yake kupitia hati hizo kutokana na baadhi ya wananchi kukiuka sheria.
“Hili nimeshaligundua kuna watu wengi wamepewa hati za muda na wamewekeza, kisheria ardhi yote ambayo ni kitega uchumi ni lazima upewe hati ya kukodishwa ardhi au lend lise ili kuona kwa mujibu wa ukubwa wa eneo uwe unalipa serikalini,” alifafanua.
Alisema kama wizara yake imelivalia njuga na ameshaanza kulifanyia kazi kuona kila mwenye hati ya muda basi anawajibika kwa kufuata sheria za ardhi.
Alisema matatizo ya ardhi yapo mengi kwani wapo baadhi ya watu katika eneo la Kilimani katika sehemu za kibiashara wamepewa hati za muda hivyo ni lazima kuwajibika kwa mujibu wa sheria.