NEW YORK, MAREKANI

SHIRIKA la biashara duniani limeitisha mkutano wa mawaziri wa biashara kwa lengo la kuhimiza mazungumzo ya muda mrefu yenye lengo la kupiga marufu ruzuku zinatolewa kwa wavuvi wanaovua kupita kiasi.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Ngozi Okonjo-Iweala ameelezea matumaini kwamba mawaziri wataokutana kutoka nchi wanachama 164 wa shirika la WTO watafanikiwa kufikia makubaliano ya kihistoria.

Amesema bahari na sayari ya dunia zimo katika hali mbaya na kwamba mawaziri hao wanapaswa kuitumia fursa ya mkutano huo.

Lengo la mazungumzo kwenye mkutano wa mawaziri hao wa biashara ni kufikia makubaliano juu ya kupiga marufuku ruzuku zinazochangia katika uvuvi wa kinyume cha sheria na uvuvi holela.

Kwa mujibu wa shirika la WTO ruzuku zinazotolewa kila mwaka zinafikia kati ya dola bilioni 14 hadi bilioni 54.