UNESCO yauweka katika urithi wa dunia
NA MWANDISHI WETU
UKIWA kwa mbali unapepewa na Upepo mwanana wa bahari, mandhari manzuri ya kisiwa cha kijani kibichi, Majengo ya ghorofa ambayo yanaonekana kujengwa kwa mawe.
Aidha milango iliyonakshiwa kwa ustadi mzuri (Zanzibar door), Chochoro za Mji huo utadhani kama unazunguka eneo hilo hilo moja, kumbe tayari umesogea sehemu nyengine, utembeapo maeneo hayo utashuhudia upekee wa kisiwa cha Unguja.
Hicho si kisiwa chengine bali ni kisiwa cha Unguja kisiwa ambacho kimebarikiwa vivutio vingi ambavyo humburudisha mtembeajii na sehemu vilivyopo vivutio hivyo ni pamoja na Mji Mkongwe.
Ukiwa ndani ya Mji huo utajikuta unafaidika kwa namna mbili, ambayo ni matembezi ama utalii wa ndani na matembezi ya utalii wa nje, ila matembezi ya Mji Mkongwe kwa jina la kigeni hujulikana kama ni Matembezi ya Mji (CityTour)
Ni matembezi ambayo huanza majira ya saa 8:30 asubuhi kuzunguka Mji Mkongwe wote, na huchukua masaa mawili hadi matatu kushuhudia maajabu mengi ya kisiwa cha Unguja ambayo humvutia mtembeaji kwa kujionea kwa macho, bila shaka ndani yake kuna vivutio vingi na ndio fahari ya Zanzibar.
Fahari ambayo, humuwezesha mtembeaji kuona umahari wa mji wa Zanzibar. Ulivyokuwa na haiba ya kipekee kupitia historia ya maeneo husika , uhalisia wa maeneo hayo kwa mfano umbile na sura ya majengo hayo au milango alisema mtembeza watalii wa kujitolea”, Habib Omar.
Bila shaka, kufanikisha matembezi ya Mji Mkongwe lazima kuwe na muongozaji wa matembezi hayo, ambaye hujulikana kama ni Mtembezaji watalii (Tour Guider), Mtembezaji huyu hujitolea ama kutoka kwenye mashirika yanayojishughulisha na kazi hii ambayo hufuata taratibu zote za msingi ya kisheria ili kuepuka usumbufu.
Kwa hivyo, Makala hii itazungumzia vivutio vinavyopatikana katika matembezi ya Mji (City Tour).
Miongoni mwa vivutio ambavyo mtalii hupaswa kuviona ndani ya matembezi ya Mji (City Tour) ni kama vifuatavyo Soko la Darajani, Makumbusho ya Amani (Peace Memorial), Kanisa (Anglican Cathedral Christ Church), Bwawa la Hamamni (Hamamni Persian Baths), Ngome kongwe (Old Fort), Forodani (Forodhan Park), Jumba la Ajabu(Beit-al-ajab , House of Wonder ) na Makumbusho ya kikasri (Palace Museum).
SOKO LA DARAJANI.
Soko la darajani limejengwa mnamo mwaka 1904, kwa kawaida soko hili hujumuisha bidhaa za namna nyingi na mara nyingi bidhaa za sokoni hapo huwa ni mpya kutoka shambani, utashangaa muda mwengine kuona vitu bado vipo kati tayari vishatoka kwenye msimu wake na ni sehemu nzuri ya kununua bidhaa mbali mbali na kujionea mazingira.
Watu hutokea maeneo mbali mbali ya Zanzibar kuleta bidhaa zao na wengine kununua bidhaa hizo Biashara, wauzaji, wanunuzi, wote hujumuika pamoja katika kufanikisha shughuli za kisoko.
KANISA (ANGLICAN CATHEDRAL CHRIST CHURCH)
Ni alama ya kihistoria ambayo huonesha uwepo wa ukiristo visawani Zanzibar limejengwa miaka 10 tokea mwaka 1873 na lipo Mkunazini mjini Unguja.
Edward Streere ni askofu wa watatu wa kanisa hilo, ndiye aliyechangia usarifu wa ramani ya jengo la kanisa mpaka kujengwa.
Kanisa hilo limejengwa kwa madhumuni ya kumaliza biashara ya utumwa ilioshamiri katika kipindi hicho.
Hadi sasa uingiapo kanisani hapo pana shimo kubwa na masanamu yaliyofungwa minyororo kuonesha uhalisia wa watumwa wanavyokuwa sokoni miaka hiyo.