NA ASYA HASSAN

PAMOJA na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kukemea vitendo vya rushwa na ubadhirifu, bado wapo baadhi ya watumishi wa umma wanaendeleza vitendo hivyo.

Hayo yamejiri baada ya Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhuijumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), kuwashikilia watu 11 ambao inawatuhumu kuhusika na michongo ya kujipatia fedha kwa njia ya wizi na ubadhirifu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ahmed Khamis Makarani akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake katika bustani ya Victoria, alisema ZAECA inawashikilia watu kwa tuhuma za kutengeneza vyeti bandia vyenye matokeo ya upimaji wa ugonjwa wa corona kwa wasafiri.

Alisema kwa kutengeneza vyeti hivyo, watu hao walikuwa walikuwa wakijipatia mali fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha kuitia hasara serikali zaidi ya dola 50,000.

Mkurugenzi huyo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na Rashid Saleh (32) mkaazi wa Michenzani, ambaye ni mfanyakazi wa taasisi ya kusaidia mayatima, Peter Masika Wafula (41) raia wa Kenya anaishi Kwa Mchina ambae anafanya kazi katika hospitali ya Al Rahma.

Wengine Hassan Vuai Hassan (41) Kwarara anafanyakazi wizara ya Afya sehemu ya maabara, Yassir Said Ali (27) mkaazi wa Tomondo ambae ni mfanyakazi wa kujitolea ZACP katika kitengo cha COVID 19, Jamal Abbas Abdalla (38) anaishi Kilimani mfanyakazi wa Uwanja wa Ndege, Abdalla Mohammed Juma (25) mfanyabiashara na sekta ya utalii.

Asya Gharib Haji (39) mkaazi wa Mpendae mfanyakazi wa wizara ya Afya maabara, Salum Haroub Amour (24), mkaazi wa Miembeni mfanyakazi wa Bohari Maruhubi (Part time), Arafa Abdul-hakim Muhsin (30), mfanyakazi wa wizara ya Afya kitengo cha COVID 19, Mbarouk Khamis Ali (43) Masingini mfanyakazi wa wizara ya afya maabara na Hussein Ame Haji ambae ni mfanyakazi wa kitengo cha COVID 19 makao makuu.

Alitaja idadi ya waliopewa vyeti kwa njia ni vyeti 548 ambayo wamepewa wasafiri aliotoka Zanzibar kwenda sehemu mbalimbali duniani.

Makarani alisema kwa bahati mbaya sana katika idadi ya waliopewa vyeti kuthibitisha kuwa wamepimwa corona pia inajumuisha baadhi ya viongozi wa juu serikalini.