NA ASYA HASSAN

MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), imesema maendeleo ya Zanzibar yatafikiwa endapo kutakuwa na udhibiti mpana wa vitendo vya rushwa kupitia sekta za kimaendeleo.

Mkurugenzi Kinga dhidi ya Rushwa wa mamlaka hiyo, Makame Khamis Hassan, alieleza hayo jana ofisini kwake Victoria Garden alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya rushwa Afrika inayoadhimishwa Julai 11 ya kila mwaka.

Alisema kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo kupitia maeneo kunasababisha kuviza maendeleo ndani ya visiwa hivi na kuwafanya wananchi wake kuendelea kuwa maskini kutokana na kukosekana kwa huduma nyingi za kijamii.

Alifahamisha kwamba katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021, mamlaka hiyo ilipokea malalamiko 382 kati ya hayo 280 ni tuhuma ambazo zinaendelea kufanyiwa uchunguzi na tuhuma 59 zimefungwa baada ya kukosekana ushahidi.

Makame aliongeza kuwa majalada 29 yamefikishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria na majalada 18 yamehamishiwa kwenye taasisi zinazohusiana na tuhuma hizo.

Aidha Mkurugenzi huyo alifafanua kwamba tuhuma 15 zimefanyiwa udhibiti kutokana na kutokamilika ushahidi ili kutoa njia sahihi za kiutendaji katika sekta husika, huku tuhuma 33 zimetolewa ushauri na tuhuma tano zimewasilishwa mahakamani na kesi nne zimetolewa maamuzi.

“Miongoni mwa tuhuma hizo kuna zile zinazohusisha miradi mbali mbali ukiwemo ZUSP, tuhuma zinazohusu vikosi vya SMZ kama vile JKU, Kikosi cha Zima Moto na Uokozi, Kesi zinazohusu Wizara ya Fedha, Jumba la Treni, ZECO, MASTERLIFE, Manunuzi hewa ya mbolea ya Urea,” alisema.

Alifahamisha kwamba katika maeneo hayo kuna tuhuma tofauti ikiwemo kufanya ubadhirifu wa mali na mapato, matumizi mabaya ya ofisi, kutokufuata taratibu za manunuzi, kukwepa kulipa kodi ambapo uchunguzi wa majalada ya kesi hizi unaendelea.

Mbali na hayo Mkurugenzi huyo alisema kwa kipindi kama hicho mamlaka hiyo imefanikiwa kuokoa jumla ya shilingi 411,348,724.30 ambazo zilikuwa zitumike kinyume na utaratibu.