NA MWAJUMA JUMA

CHAMA cha Makocha wa Mpira wa Miguu Zanzibar (ZAFCA) kimesema ujio wa rais wa mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), utafungua ukurasa mpya kwa makocha hasa katika suala zima la elimu kwa ngazi zote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu wa chama hicho Ibrahim Makeresa alisema chama chao, kimefarijika sana kupata rais huyo na kusema watashirikiana nae hatua kwa hatua kuendeleza soka la Zanzibar.

Alisema  matumaini yao rais huyo atakuwa mstari wa mbele katika kuwaendeleza makocha wao, ili kuhakikisha kwamba Zanzibar wanaongeza idadi ya makocha bora katika tasnia ya soka.

“Tuna matumaini makubwa sana kwamba mashirikiano yetu  makocha na wadau wengine wa mpira wa miguu yataweza kutufikisha mbali Zanzibar katika mpira wa miguu’’alisema.

Sambamba na hayo alisema watatoa ushirikiano wa kutosha kwa rais huyo katika kuimarisha soka la Zanzibar, hususan katika masuala ya kiufundi katika idara mbali mbali zinzohusiana na ufundi ikiwemo makocha.

Abdul-latif alichaguliwa  kwa kupata kura 16 kati ya 24 zilizopigwa na kumpita mpinzani wake Suleiman Shaaba ambae alipata kura nane.