NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Real Kids imeshindwa kutamba mbele ya ZAFSA kwa kukubali kichapo cha bao 1-0, katika mchezo wa ligi daraja la tatu wilaya ya mjini hatua ya sita bora.

Mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong ulikuwa na ushindani mkali huku Real Kids ambao ndio wenyeji wa mchezo huo wakijilaumu kwa kukosa mabao mengi ya wazi.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilicheza kwa kukamiana huku ZAFSA ambao walikuwa na ngoma ya dufu walijiamini vilivyo na kufanikiwa kutia bao katika dakika ya tisa tu ya mchezo huo kupitia kwa Mundhir Makame Suleiman.

Ligi hiyo leo inatarajiwa kuendelea tena kwa mchezo utakaowakutanisha majirani wa karibu timu za Kwamtipura na Ziwatuwe, mchezo ambao utachezwa katika uwanja wa Mao Zedong A saa 10:00 za jioni.