BAGHDAD, IRAQ
TAKRIBANI watu 50 wamefariki na wengine zaidi ya 60 wamejeruhiwa baada ya moto kuzuka katika hospitali ya Imam al-Hussein inayotumiwa na wagonjwa wa Covid-19 kwenye mji wa Nassiriya nchini Iraq.
Maafisa wa afya katika mji huo ulioko kwenye jimbo la Dhi Qar, wamesema moto huo uliotokea jana usiku umesababishwa na kuripuka kwa mtungi wa gesi.
Msemaji wa idara ya afya katika jimbo hilo, Ammar Bashar amesema miili 41 imepatikana baada ya moto huo kuzimwa.
Aidha Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amefanya mkutano wa dharura wa mawaziri na makamanda wakuu wa usalama kujadiliana kuhusu mkasa huo.
Inaelezwa kuwa mfumo wa afya wa Iraq umekuwa ukipambana na kukabiliana na janga la virusi vya corona ambalo limewaua watu 17,592 na wengine zaidi ya milioni 1.4 wakiwa wameambukizwa virusi hivyo.