NA AMEIR KHALID, MTWARA

TIMU za mpira wa mikono wanaume Unguja na soka kanda ya Pemba, na mpira wa Kikapu zimefanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya UMISSETA, yanayoendelea mkoani Mtwara.

Wanaume mikono wamefika hatua hiyo baada ya kushinda mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya mkoa Morogoro kwa kuifunga mabao 25 – 12.

Kwa upande wa riadha kanda ya Unguja imefanikiwa kupata medali 10 kwa kichezo yote jumla yake.

Wanaume wamepata medali nne za dhahabu katika michezo ya kurusha tufe, kisahani, mbio za kupokezana vijiti ndogo na kubwa, medali ya fedha mbio za mita 200, shaba mbio za mita 100 na 200.

Wanawake wamepata medali za fedha kwa mchezo wa kurusha kisahani na mkuki, wakati medali ya shaba wameipata kwa kurusha tufe.

Timu ya mpira wa kikapu nayo imeingia hatua ya fainali baada ya kutoka na ushindi wa pointi 63 – 57 dhidi ya mkoa wa Mwanza, mchezo ambao ulikuwa mgumu kwa muda wote kwani licha ya kupoteza Mwanza ilitoa upinzani mkubwa kwa Unguja.

Kwa upande wa timu ya mpira wa Wavu imeshindwa kuingia hatua ya fainali baada ya kufungwa seti 3-2 na mkoa wa Dar es Salaam.

Leo kutapigwa fainali ya mpira wa mikono wanaume ambapo Unguja itacheza na mkoa wa Tabora, kikapu itacheza na mkoa kati ya Morogoro na Dar es Salaam, soka Pemba itacheza wenyeji Mtwara.

Mechi za kutafuta mshindi wa tatu Wavu Unguja itacheza kati ya Tabora au Arusha, wanawake mikono watacheza na mkoa wa Geita.