NA HAFSA GOLO
TATIZO la maradhi kwa wanyama Zanzibar hasa wa biashara limepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita hivi karibuni kutokana na wafugaji kuwa na mwamko wa kufuata masharti na maelekezo ya wataalamu nchini.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Asha Zaharani Mohammed, alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Maruhubi nje kidogo ya mji wa Unguja.
Alisema sababu kubwa ya kupungua kwa tatizo hilo, limechangiwa na wafugaji wa wanyama wa Kuku, Ng’ombe na Mbuzi , kujenga utamaduni endelevu wa kutumia kinga kuliko tiba.
Aidha alisema, hatua hiyo ipo pamoja na wafugaji hao kufuata ipasavyo mbinu za kisasa za ufugaji zinazoelekezwa na wataalamu ambazo zimekuwa zikichangia kiasi kikubwa kuleta tija na kufikia malengo ya wafugaji.
“Hii imechangiwa na wafugaji kuweka mazingira bora na salama ya makaazi ya wanyama wao huku wakisimamia taratibu na maelekezo ya wataalamu wa mifugo”,alisema.
Nae Daktari Mkuu wa Mifugo Zanzibar, Dk. Talib Saleh Suleiman, alisema, miongoni mwa maradhi ya wanyama yaliopungua kwa asilimia 90 ni pamoja na ugonjwa wa miguu , midomo na kimeta cha mbavu.